Kundi moja linalohusika na masuala ya ukimwi katika Umoja wa Mataifa lilitangaza Alhamis kwamba watengenezaji wa dawa za ukimwi wataanza kutengeneza vidonge vya gharama nafuu kwa wagonjwa wa ukimwi wa Afrika kwa ufadhili kutoka taasisi ya hisani ya Bill Gates.
Taasisi ya Gates itahakikisha uuzaji wa vidonge vya idadi ya wastani na kupelekea watengenezaji madawa wa Mylan Laboratories na Aurobindo Pharma wakubali kuweka gharama ya matibabu kwa mgonjwa iwe dola 75 kwa mwaka. Dawa ya bei ya chini ya ukimwi itapatikana kwa ununuzi utakaofanywa na taasisi za sekta za umma mwaka ujao na makadirio yanaonesha ushirika huo utaokoa zaidi ya dola bilioni moja katika gharama za afya kwa kipindi cha miaka sita ijayo.
Tangazo hilo limetolewa kwenye mkutano wa UNAIDS ambao unalenga kutokomeza virusi vya HIV. UNAIDS inatoa wito kwa nchi kuongeza viwango vyao vya utoaji huduma za HIV katika juhudi za kumaliza mlipuko wa ugonjwa wa ukimwi ifikapo mwaka 2030.