Sudan Kusini imetangaza janga la kibinadamu katika jimbo la Jonglei eneo ambalo limekuwa na mapigano ya mara kwa mara ambayo yameuwa mamia ya watu.
Msemaji wa serikali amesema baraza la mawaziri Sudan Kusini limetangaza janga hilo katika mkutano maalum jana na kuyaomba mashirika ya misaada ya kimataifa kupeleka msaada haraka kwenye jimbo hilo.
Kundi la wapiganaji 6000 kutoka kabila la Lou Nuer lilishambulia miji ya Lukangol na Pibor wiki iliyopita, na kuchoma moto mahema na kusababisha maelfu kukimbia eneo hilo. Pibor ndio eneo wanalotoka watu wa kabila la Murle, ambao wanashutumiwa kwa mashambulizi kwenye eneo la Lou-Nuer mwezi Agosti.
Serikali inasema majeshi yake yameidhibiti Pibor na kusema itajaribu kuandaa mazungumzo ya maridhiano kati ya makabila hayo.