Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 23:14

Sudan kuanza mazungumzo ya ushirikiano na Israel


Waziri mkuu wa Sudan Abdallah Hamdock
Waziri mkuu wa Sudan Abdallah Hamdock

Hatua hiyo ni ishara ya uwezekano wa kurejesha uhusiano wa kawaida  kati ya Israel na Sudan baada ya miongo kadhaa ya migororo baina ya nchi hizo mbili.

Wizara ya mambo ya nje ya Sudan imesema kwamba Sudan na Israel zitajadiliana kuhusu makubaliano ya ushirikiano wa kibiashara na uhamiaji, katika wiki za karibuni.

Hatua hiyo ni ishara ya uwezekano wa kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Israel na Sudan baada ya miongo kadhaa ya migororo baina ya nchi hizo mbili.

Mkataba wa uhusiano bora kati ya Sudan na Israel, uliosimamiwa na Marekani, umeifanya serikali ya Khartoum kuwa ni serikali ya tatu ya kiarabu kurejesha uhusiano na Israel katika kipindi cha miezi miwili, na mkataba huo unakuwa wa tano tangu mwaka 1948.

Lakini makundi maarufu ya wanasiasa nchini Sudan yameupinga mkataba huo.

Baadhi ya maafisa wa Sudan wamesema kwamba mkataba huo unastahili kupitishwa na bunge la serikali ya mpito ambalo halijaundwa baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa maandamano yaliyomuondoa madarakani Omar al-Bashir.

Wizara ya mambo ya nje ya Khartoum imesema kwamba wajumbe wa Sudan na Israel watakutana katika muda wa wiki chache zijazo, kujadiliana kuhusu uwezekano wa kupatikana mkataba wa kibiashara, kilimo na uhamiaji.

Taarifa ya wizara hiyo haijatoa maelezo zaidi kuhusu muda ambao mazungumzo hayo yatachukua kumalizika.

Zaidi ya raia wa Sudan 6,200 wanaishi nchini Israel na wanaaminika kuingia nchini humo kinyume cha sheria kwa sababu za kiuchumi.

Hatua ya kuwarejesha nyumbani raia hao wa Sudan, imepata pingamizi kubwa kutokana na uhusiano mbaya kati ya nchi hizo mbili, pamoja na changamoto za kisheria katika mahakama za Israel.

“Naelewa kwamba tayari wamekubaliana kuhusu mpango wa majaribio wa kuwarejesha mamia ya watu katika siku chache zijazo ,” amesema waziri wa nshati wa Israel, Yuval Steinitz katika mahojiano na televisheni ya Ynet.

Steinitz ameongezea kwamba “nafikiri kwamba baada ya mamia hao kurudi makwao, maelfu watafuata.”

Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya ndani ya Israel ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba hawajui chochote kuhusu mpango huo.

Mchakato wa kurejesha uhusiano kati ya Israel na Sudan ni swala ambalo limezua hisia kali sana nchini Sudan, ambayo imekuwa mkosoaji mkali sana wa Israel.

Swala hilo limesababisha mipasuko kati ya wanajeshi pamoja na viongozi wa kiraia wakati nchi hiyo inajaribu kurejesha hali ya utulivu baada ya utawala wa rais wa zamani Omar al-Bashir.

Waziri mkuu wa Sudan anataka mkataba huo kuidhinishwa na bunge ambalo halijaundwa, na ambalo uundwaji wake unaweza kuchukua muda kutokana na misimamo tofauti kati ya viongozi wa kijeshi na kiraia kuhusu ushirikiano na Israel.

Haijulikani ni lini bunge hilo litaundwa, ambalo ni sehemu ya mchakato wa serikali ya mpito katika kuandaa uchaguzi ulio huru na haki.

Ripoti ya ujasusi ya Israel iliyotolewa Oktoba 15, ilibashiri uwezekano wa kufikia makubaliano na Sudan, kuhusu kilimo na kuboresha mahusiano kati ya nchi hizo mbili.

Ripoti hiyo vile vile inataka ushirikiano na Sudan katika kumaliza kile ilichokitaja kama kukomesha maadui wa Israel kama Iran na Hamas, kutumia ardhi ya Sudan.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG