Sudan itamkabidhi kiongozi wa muda mrefu nchini humo, Omar al-Bashir kwa mahakama ya kimataifa ya uhalifu (ICC) pamoja na maafisa wengine wanaotafutwa juu ya mzozo wa Darfur, waziri wa mambo ya nje wa Sudan, Mariam al-Mahdi alisema Jumatano.
Baraza la mawaziri liliamua kuwakabidhi maafisa wanaotakiwa na ICC, Mahdi alinukuliwa na vyombo vya habari vya serikali. Bashir ambaye alitawala Sudan kimabavu kwa miongo mitatu, kabla ya kuondolewa madarakani kufuatia maandamano makubwa yaliyopata umaarufu mwaka 2019 anakabiliwa na mashtaka ya mauaji ya kimbari, uhalifu wa vita, na uhalifu dhidi ya binadamu huko Darfur.
Umoja wa Mataifa unasema watu laki tatu waliuawa na wengine milioni 2.5 walikoseshwa makazi yao katika mzozo huo ambao ulizuka katika eneo kubwa la magharibi mwaka 2003.
Bashir mwenye miaka 77 amekuwa akitafutwa na ICC tangu mwaka 2009 wakati ilipotolewa hati ya kukamatwa kwake. Uamuzi wa kumkabidhi ulikuja wakati wa ziara ya Sudan ya mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Karim Khan.