Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 16:12

Dr Nyanzi awekwa rumande kwa madai ya kumdhalilisha Museveni


Rais Museveni na mkewe Janeti
Rais Museveni na mkewe Janeti

Mtafiti wa saikolojia na jinsia katika chuo kikuu cha mekerere Dr Stella Nyanzi, anazuiliwa katika gereza la Luzira jijini Kampala kwa madai ya kumtusi na kumdhalilisha rais Yoweri Museveni, akimlinganisha na makalio. Kupitia mtandao wa kijamii wa facebook Dr Nyanzi alimdhalilisha pia mke wa rais.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa kuzuiliwa gerezani kwa Dr.Stella Nyanzi ambaye amekuwa mkosoaji wa serikali yake Museveni, kunajiri baada ya kukamatwa katika mazingira ya kisiri, kuzuiliwa wikendi nzima bila maelezo, na baadaye kuwasilishwa mahakamani.

Mbele ya jaji wa mahakama ya Buganda jijini Kampala, Eremye Mawanda, upande wa mashtaka ukiongozwa na Jonathan Mugwanya umemtaka jaji kumzuilia Dr. Nyanzi na kutaka apimwe akili kubaini iwapo ana matatizo yoyote ya kiakili, kwa

kumtusi rais na mke wake bila kuogopa, si jambo la kawaida, huku mawakili wa mshtakiwa wakiongozwa na Nicholas Opiyo wakipinga ombi la serikali, wakidai kwamba hatua ya kumpima mteja wao akili, pia ni hatua ya kumdhalilisha.

Dr. Nyanzi amekuwa akiikosoa serikali kupitia mitandao ya kijamii, akitaka serikali kutoa visodo yani pamba maalumu zinazotumiwa na wanawake kwa wanafunzi katika shule za msingi bila malipo. Na aliposomewa mashtaka ya kumfananisha rais museveni na makalio, hakuwa mwenye maneno yenye upole

‘Ni kweli nimeandika sana kuhusu mambo mengi jaji mheshimiwa. Nimeandika kuwahusu wanaotutawala, utawala wa kifamilia, utawala wa kijamii na mambo ambayo si mazuri kwa wale wanaowadhulumu raia.

Lakini, sina makosa ya kumuudhi yeyote’ Dr Nyanzi ameeleza mahakama, akiendelea kusema kwamba serikali yake Museveni imewakandamiza raia wa Uganda kwa muda mrefu.

Kukosea kuna maana gani? Waganda wamekosewa sana na utawala uliopo. Nani anamkosea mwingine. Mwanamke Anayesema ukweli anaambiwa amekosa? Ni mara ngapi rais museveni amekosea nchi hii? Waganda wataendelea kuishi kwa uoga hadi lini kwa sababu wanaogopa kufunguliwa mashataka ya kukosea.

Nyanzi aliwahi kuvua nguo na kubaki kifua wazi mnamo mwaka jana, chuo kikuu cha makerere kilipotaka kumtimua katika nafasi yake ya kuwa mmoja wa watafiti wakuu wa chuo kikuu cha mekerere kwa kuikosoa serikali. Amewahi pia kumtusi mke wa rais Museveni, kwa kutumia lugha chafu akimfananisha na sehemu za siri za maumbile ya kike.

Mitandao ya kijamii imejaa hisia za waganda kuhusu kukamatwa na kuzuiliwa kwa mtafiti huyo wa maswala ya kisaikolojia na jinsia, wengi wakimuunga mkono kwa msingi kwamba hata rais Museveni amekuwa na mazoea ya kutumia lugha chafu dhidi ya wapinzani wake.

Mshitakiwa, aliye na ufuasi mkubwa kwenye mitandao ya kijamii, atarejeshwa mahakamani tarehe 25 mwezi huu.

XS
SM
MD
LG