Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:02

Spika wa Bunge la Tanzania Job Ndugai ajiuzulu


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam, Tanzania.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai. Picha kwa hisani ya Ikulu ya Dar es Salaam, Tanzania.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amejiuzulu nafasi yake Alhamisi, siku tatu baada ya kumuomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan kwa matamkshi yake ya kuikosoa serikali kuendelea kukopa.

Katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari, Ndugai amesema alikuwa amekiandikia chama chake, Chama cha Mapinduzi (CCM) juu ya “uamuzi wake binafsi” wa kujiuzulu kama spika.

“Naomba kutoa taarifa kwa umma wa Watanzania kuwa leo tarehe 06, Januari, 2022 nimeandika barua kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kujiuzulu nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Uamuzi huu ni binafsi na hiari na nimeufanya kwa kuzingatia na kujali maslahi mapana zaidi ya taifa langu, serikali na chama changu cha CCM.

Chanzo cha sakata la mkopo

Chanzo cha migongano ni kauli zilizotolewa na spika kuhusu mkopo uliopokelewa na serikali ya Tanzania kutoka Shirika la Fedha Duniani (IFM) wa shilingi trilioni 1.3, fedha ambazo zinatumika kwa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, vituo vya afya na huduma nyinginezo.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania

Akizungumza jijini Dodoma, Desemba 27, 2021, Job Ndugai alionekana kumlenga moja kwa moja Rais Samia kwa kusema, "Juzi mama ameenda kukopa shilingi trilioni 1.3.

Ndugai alisema: “Hivi ipi bora, sisi Watanzania kwa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa tuwe na madeni au tubanane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe na kwa namna gani? Tutembeze bakuli ndio heshima? Tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku? Tukasema pitisha tozo anayetaka asiyetaka, pitisha tozo lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyie, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.”

Aliendelea kusema “Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo sawa, waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo nayo ni namna ya kuongoza nchi, hivi sasa deni letu ni Trilioni 70. Hivi nyinyi wasomi hiyo ni afya kwa taifa? Kuna siku nchi itapigwa mnada hii."

Siku moja baadaye Rais Samia alijibu, na kusisitiza kwamba serikali itakopa kugharamia miradi ya maendeleo.

"Kwa njia yoyote, kwa vyovyote tutakopa.Tutaangalia njia rahisi, njia zitakazotufaa kukopa na fedha hizi hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani, ni lazima tutakopa.

Kama walidhani kutakuwa kuna kusimamishwa miradi ili wapate la kusema, halipo. Kuna jitihada za kutuvunja moyo kwenye mkopo, hakuna nchi isiyokopa, tutakopa tumalize miradi ya maendeleo ili tuendelee kwa sababu ukikopa unajenga sasa kwa haraka na kuharakisha maendeleo na mikopo hii ni ya miaka 20 kwahiyo tutakopa na tutalipa taratibu," alisema Rais Samia.

XS
SM
MD
LG