Mamlaka nchini Kenya yanaendelea kuwachunguza na kuwatimua kazini maafisa wa usalama wanaojihusisha na uhalifu, au kushirikiana na magenge ya ujambazi yanayohangaisha au hata kuuwa raia.
Katika miji ya Nairobi na Mombasa, pwani ya Kenya maafisa kadhaa wa usalama wamesimamishwa kazi, kwa madai ya kutoa mafunzo ya kivita kwa magenge ya wahalifu.
Wakazi wa pwani hasa, wamekuwa wakiishi kwa hali ya wasi wasi hasa kutokana na kuwa kuna makundi mengi ya ujambazi katika eneo hilo na kwa hivyo taarifa kuwa baadhi ya maafisa wa usalama huenda wanashirikiana nao kumeongeza wasi wasi huo hata zaidi.