Hii ni baada ya kuongezeka kwa mashambulizi, kuwazuia wagombea wa chama tawala na wafuasi wao kuandaa mikutano ya kampeni katika miji kadhaa.
Tume ya uchaguzi ya taifa nchini Chad, ANGE, imesema kampeni kuelekea uchaguzi wa bunge na serikali za mitaa, Desemba 29 zimegubikwa na matukio ya ghasia dhidi ya wagombea na maafisa wa uchaguzi.
Maafisa wa Chad wanasema uchaguzi huo utafikisha kikomo miaka mitatu ya serikali ya mpito kufuatia kifo cha rais wa muda mrefu Idriss Deby Into, mwezi April 2021.
Assane Bairra ni makamu mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya Chad.
“Tume ya uchaguzi imeomba msaada wa jeshi kuwalinda raia, wagombea na maafisa wa tume ya uchaguzi na waangalizi wa kimataifa wakati na baada ya uchaguzi wa Desemba 29. Hali ya wasiwasi inayoendelea huenda ikageuka na kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe iwapo jeshi halitaingilia kati kuwalinda wagombea na wafuasi wao katika kampeni.”
Tume ya uchaguzi imesema zaidi ya watu milioni 8.3 kati ya jumla ya watu wote milioni 18, wamejiandikisha kupiga kura.
Idadi kubwa ya wagombea
Karibu vyama vya siasa 180 vimewasilisha wagombea 1,300 kuwania viti 188 vya bunge la taifa pekee.
Maelfu ya wagombea wengine wanaowania nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa serikali za mitaa na mikoa.
Kuna zaidi ya waangalizi wa uchaguzi 1000.
Hata hivyo, muungano wa vyama vya upinzani 75 na makundi ya kutetea haki za kiraia, wameutaja uchaguzi huo kuwa wenye njama fiche, wakidai kwamba rais wa Chad Mahamat Idriss Deby na chama chake cha Patriotic Salvation Movement, au wabunge wanapanga kutumia uchaguzi huo kung’ang’ania Madaraka.
Makundi ya upinzani na ya kijamii yanasema wafuasi wao wametumia marungu na vyuma kuwashambulia wabunge wanaofanya kampeni katika miji kadhaa, ikiwemo Ndjamena, Bongor, Abeche, Lai na Moundou.
Katika baadhi ya sehemu, jeshi limesema limeharibu vizuizi barabarani vilivyokuwa vimewekwa na wafuasi wa vyama vya upinzani kuwazuia wabunge wanaofanya kampeni kuingia katika miji hiyo.
Avocksouma Djona, ni kiongozi wa chama cha Chad party of democrats.
“Chama chetu kinataka uchaguzi uahirishwe kwa sababu maafisa wote wa uchaguzi wameteuliwa na Deby ambaye ametawala kimabavu na mtoto wake wa kiume hayupo tayari kuleta demokrasia nchini Chad. Deby anaongoza mahakama ya katiba na amewaamuru majaji kuamua kwamba chama chake kimeshinda uchaguzi.”
Tume ya uchaguzi ya Chad, ANGE huandaa uchaguzi na kutangaza matokeo kulingana na sheria za Chad.
Madai ya Deby kung'ang'ania madaraka
Deby ameteua maafisa wa tume ya uchaguzi na wa mahakama ya katiba. Aliiambia televisheni ya taifa wiki hii kwamba uchaguzi wa Chad utarudisha utawala wa kiraia na utakuwa huru na haki.
Makundi ya upizani yamefutilia mbali madai yake yakisema kwamba kiongozi huyo anapanga kufanya udanganyifu katika uchaguzi ili kuwa na idadi kubwa ya wabunge.
Deby aliteuliwa kuwa kiongozi wa mpito wa Chad mnamo April 2021 baada ya kifo cha babake Idriss Deby aliyeuawa akiwa katika vita dhidi ya waasi. Aliongoza Chad kwa muda wa miaka 30.
Alikuwa ameahidi kuongoza kipindi cha mpito cha miezi 18 lakini akajiongezea muda madarakani kwa miaka miwili.
Alishinda uchaguzi wa urais mwezi Mei, ambao vyama vingi vya upinzani vilisusia vikisema kwamba alikuwa anatumia kila mbinu kusalia madarakani na kuendeleza utawala wa babake.
Forum