Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa kituo kinachofuatilia silaha ndogo ndogo na nyepesi Kenya na kanda ya Maziwa Makuu kinasema kuwa silaha haramu 500,000 ziko mikononi mwa baadhi ya wananchi; hususan jamii ya wafugaji.
Amesema hali hiyo imeleta wasiwasi mkubwa hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi mkuu uko karibu.
Mwandishi huyo ameongeza kuwa tayari kuna mikakati mbalimbali kutoka kwa vyombo vya usalama nchini kutengeneza sheria ya kudhibiti na kuondoa uingizaji wa silaha hizo nchini, ambayo inaelekea bado ina changamoto nyingi.
Mshauri wa masuala ya silaha
Afisa na mshauri wa kituo kinachofuatilia silaha ndogo ndogo na nyepesi Kenya na kanda ya Maziwa Makuu, Francis Wairagu, anaeleza kuwa takwimu za kuwepo kwa silaha nyingi haramu nchini Kenya ni jambo ambalo linatia wasiwasi.
“Kuwepo kwa silaha ndogo ndogo na nyepesi nchini mikononi mwa baadhi ya wananchi kumekuwa na changamoto nchini kwa muda mrefu sasa,” amesema afisa huyo.
Wairagu amesema kuwa mara nyingi wakati vyombo vya usalama vinapoanza juhudi za kunasa silaha hizi haramu zilizopo mikononi mwa wananchi, kumekuwa na taarifa ya matumizi ya nguvu na vyombo vya dola kinyume cha sheria.
Lakini pia amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kufanikisha juhudi hizi.
Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu
Nchi za kanda ya Maziwa Makuu ni pamoja na Tanzania, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Kenya na Uganda.
Wasiwasi huo unatokana na ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/8 ulioifanya Kenya kuongeza juhudi za kuwanasa na kupunguza umiliki wa silaha hizi.
Tangu miaka ya sabini, nchi zinazopakana na Kenya kama vile Somalia, Sudan na Ethiopia zimekuwa zikishuhudia vipindi virefu vya machafuko na vita vya wenyewe kwa wenyewe na hivyo basi hali hii imechangia katika uingizwaji wa silaha haramu nchini Kenya.
Elizabeth Kisiigha, mkurugenzi mtendaji wa Muungano wa Ushirika wa Halmashauri ya Makanisa katika eneo la Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika ameiambia Sauti ya Amerika kuwa suala la kuwepo silaha hizi haramu si tatizo nchi moja bali limeenea katika kanda ya Maziwa Makuu na Pembe ya Afrika kwa ujumla.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennedy Wandera, Kenya