Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:20

Siasa za kumrithi Museveni, Majenerali wanajibizana


Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni
Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni

Majenerali waliosaidia rais wa Uganda Yoweri Museveni kuingia madarakani, wanaendelea kutoa hisia zao hadharani kuhusiana na tabia ya mtoto wa Museveni Generali Muhoozi Kainerugaba kuwakosoa, kukosoa chama chao cha NRM na kujihusisha na siasa.

Majenerali hao wakiongozwa na waziri wa mambo ya ndani Meja Jenerali Kahiinda Otafiire, vile vile wanataka Muhoozi kutambua kwamba walipigana sana, walimwaga damu kabla ya kuingia madarakani na kuleta kile wanataja kama demokrasia na kwamba hawataruhusu demokrasia hiyo kufa.

Akizungumza katika kipindi cha majadiliano kwenye mojawapo ya radio maarufu Uganda, CBS, Generali Otafiire, amesema kwamba majenerali waliopigana vita na kumwezesha Museveni kuongoza taifa hilo, hawataruhusu mtoto wake kuwadharau.

“Najua kwamba wewe Muhoozi ni mtoto wa rais Museveni lakini hatutakuruhusu utudharau,” amesema waziri Jenerali Kahinda Otafiire.

Otafiire amesisitiza kwamba alikuwa anazungumza kwa niaba ya majenerali wengine.

“Nazungumza kama mwanachaka wa National resistance movement NRM na kwa niaba ya chama change. Tulipigana sana na kumwaga damu ili kuleta hii demokrasia na hatutawacha mtu kuiharibu,” ameendelea kusema Otaffire.

Majenerali Otafiire na Muhoozi Kainerugaba wamejibizana hadharani

Generali Muhoozi na generali Otafiire wamekuwa wakijibizana hadharani kwa miezi kadhaa sasa, huku Muhoozi akiasema kwamba atamfuza Otafiire na majenerali wengine somo amabalo hawatasahau.

Muhoozi amekuwa akimshambulia Otafiire na wanachama wa NRM kupitia ujumbe wa twiter.

Katika mojawapo ya ujumbe wa twiter ambao baadaye alifuta, Jenerali Muhoozi aliandika kwamba “Unatuita kuwa watu wendawazimu kwa sababu tunauliza maswali ambayo hata Watoto wanaelewa vizuri. Tumfunze Otafiire na kundi lake somo ambalo hawatasahau maishani mwao. Muda wao umeisha.”

Otafiire anataka Muhoozi kustaafu kutoka jeshi la taifa kabla ya kujihusisha na siasa, na iwapo anataka kugombea urais, kulingana na sheria za nchi.

“Sina chuki yoyote na Muhoozi, lakini kama afisa ambaye bado anatumikia jeshi, hastahili kuzungumzia saisa kabisa. Siwezi kushirikiana na mtu asiyeheshimu sheria. Mfano gani huo ambao anaweka kwa maafisa wengine wa jeshi?’ ameendelea kusema Otafiire.

Siasa za kumrithi Museveni

Kuna ripoti za vyombo vya habari nchini Uganda kwamba majenerali wastafu, waliomsaidia Museveni kuingia madarakani wanataka kuwa na uwezo wa kuamua mtu atakayeongoza Uganda baada ya Museveni.

Otaffire, ni miongoni mwa majenerali ambao wanamsimamo kwamba Muhoozi Kainerugaba hafai kuwa rais.

Vyombo vya habari vinasema majenerali wengine wanaompinga Muhoozi ni pamoja na Genereali David Sejusa, Generali Henry Tumukunde na wengine waliopigana vita vya mapinduzi.

Hivi karibuni, Otafiire aliandamana na majenerali wastaafu katika mojawapo ya hafla na kusema kwamba hawataruhusu mtu yeyote kugombea urais isipokuwa rais Yoweri Museveni kuendelea kutawala Uganda.

Muhoozi ameendelea kusisitiza kwamba “anasikiliza kilio cha watu wanaotaka mabadiliko na kwamba chama cha NRM, kinachoongozwa na babake, kina watu wasiojali maslahi ya watu.”

Muhoozi ameandika ujumbe wa Twiter kwamba “anaamini mwenyezi mungu na babake rais Museveni lkini hana Imani yoyote na chama anachoongoza babake, cha NRM.”

Muhoozi amejiwekea jina la ‘standby generator’, maana yake kwamba yupo tayari kuchukua uongozi wa Uganda anapoondoka babake wakati wowote.

Otafiire kwa upande wake, amesema “hiyo ni generator iliyokufa”.

XS
SM
MD
LG