Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 19:11

Shirika la msalaba mwekundu laomba dola milioni 112 kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Morocco


Waokoaji wa Morocco wakibeba mwili kutoka kwenye vifusi katika kijiji cha N'Yacoub katika tetemeko la ardhi lililoikumba Morocco, Septemba 11, 2023.
Waokoaji wa Morocco wakibeba mwili kutoka kwenye vifusi katika kijiji cha N'Yacoub katika tetemeko la ardhi lililoikumba Morocco, Septemba 11, 2023.

Shirika la msalaba mwekundu leo limetoa wito wa msaada wa zaidi ya dola milioni 100 ili kutoa msaada unaohitajika sana nchini Morocco, siku chache baada ya tetemeko kubwa la ardhi kuua karibu watu 2,900.

“Tunatafuta msaada wa dola milioni 112 ili kuweza kusambaza mahitaji muhimu kwa wakati huu,” Caroline Holt, mkurugenzi wa shughuli za kimataifa katika Shirikisho la kimataifa la msalaba mwekundu na Mwezi Mwekundu (IFRC), amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva.

Amesema fedha hizo zinahitajika kwa ajili ya “afya, maji, usafi wa mazingira na usafi, vifaa vya misaada vya makazi na mahitaji ya msingi”, akisisitiza kwamba wanahitaji kuhakikisha wanaepuka wimbi la pili la janga.

Timu za uokoaji kutoka Morocco na nje leo zimeendelea kuchimba kwenye vifusi vya nyumba zilizobomolewa za matofali ya udongo, zikitarajia kuwapata watu ambao bado wako hai wakati wakikimbazana na muda.

Tetemeko la siku ya Ijumaa la kiwango cha 6.8 kwa kipimo cha Rikta lilikuwa kubwa sana kuwahi kutokea nchini Morocco.

Lilikuwa tetemeko baya zaidi kupiga taifa hilo la Afrika Kaskazini tangu tetemeko la mwaka 1960 ambalo liliuharibu mji wa Agadir kwenye pwani ya Atlantic na kuua kati ya watu 12,000 na 15,000.

Jumla ya watu 2,862 walifariki na zaidi ya 2,500 walijeruhiwa katika janga hilo, kulingana na idadi rasmi iliyotolewa jana Jumatatu.

Forum

XS
SM
MD
LG