Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 18:21

Serikali ya Tanzania yafungia gazeti la 'Uhuru,' watendaji wake wasimamishwa kazi


Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Serikali ya Tanzania Jumatano ilisitisha uchapishaji wa gazeti la "Uhuru" kwa kuandika kile ilichokiita habari za uongo kwamba Rais Samia Suluhu Hassan hatawania urais mwaka wa 2025.

Ndilo gazeti la kwanza kufungiwa katika uongozi wa Samia.

Gazeti hilo linamilikiwa na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka wa 1961.

Marufuku hiyo imejiri baada ya 'Uhuru' kuandika kichwa cha habari Jumatano kwenye ukurusa wa kwanza: “Sina nia ya kugombea urais mwaka wa 2021-Samia”.

Mkurugenzi wa mawasiliano na msemaji wa serikali ya Tanzania Gerson Msigwa amesema katika taarifa kwamba "Rais Samia Suluhu Hassan hajawahi kusema kwamba hana nia ya kugombea urais mwaka wa 2025”.

Samia alichukua hatamu za uongozi mwezi Machi mwaka huu kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Pombe Magufuli.

Mwezi Aprili mwaka huu, alisema serikali itaviruhusu vyombo vya habari vilivyopigwa marufuku wakati wa enzi ya Rais Magufuli kufanya tena kazi. Muda mfupi baadaye, maafisa walifafanua kwamba televisheni za mtandaoni ndizo zingenufaika na hatua hiyo, lakini magazeti yaliyopigwa marufuku yanaweza kuomba kusajiliwa tena, na kurejeshewa leseni zao.

CCM imesema bodi ya 'Uhuru' imewasimamisha kazi maafisa wakuu watatu wanaosimamia gazeti hilo, pamoja na mkurugenzi mtendaji juu ya habari hiyo.

"Chama kinafanya uchunguzi kujua kilichotokea," katibu mkuu wa CCM, Daniel Chongolo aliwambia waandishi wa habari Jumatano.

Msigwa alisema marufuku hiyo itadumu kwa muda wa siku 14 na gazeti la hilo linaweza kukata rufaa kwenye wizara ya habari.

XS
SM
MD
LG