Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 19:54

Serikali ya Gbagbo yataka wafaransa waondoke.


Moshi ukionekana kati kati ya mji wa Abidjan.
Moshi ukionekana kati kati ya mji wa Abidjan.

Wafaransa wamechukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa Abidjan baada ya majeshi ya Gbagbo kusalimu amri.

Ivory Coast imesema jumapili kuwa majeshi ya Ufaransa hayana haki ya kuchukua udhibiti wa uwanja wa ndege katika mji mkuu wa kibiashara wa Abidjan wakati ambapo mapigano yanazidi kuongezeka baina ya serikali hiyo na wapiganaji wanaomtii mshindi anayetambuliwa kimataifa wa uchaguzi wa urais wa mwezi Novemba Alassane Ouattara.

Mwandishi wa VOA Scott Stearns anaripoti kutoka mji wa Noe ulio mpakani mwa Ivory Coast kuwa majeshi hayo ya Ufaransa yamechukua udhibiti wa uwanja wa ndege wa Abidjan baada ya majeshi yanayomtii rais anayeng’ang’ania madaraka Laurent Gbagbo kusalimu amri kwa majeshi ya Umoja wa Mataifa. Ufaransa inatumia uwanja huo wa ndege kuwasafirisha raia wa kigeni wanaotaka kuondoka nchini humo na pia kuingiza zaidi ya wanajeshi 300 kuimarisha hali katika mji mkuu huo wa kibiashara.

Mshauri wa serikali ya Gbagbo mwenye makazi yake jijini Paris, Alain Toussaint, amesema majeshi ya Ufaransa yamekuwa kama wavamizi wasio na haki ya kufanya hivyo kwa kuwa Umoja wa Mataifa haujaidhinisha majeshi hayo kutwaa uwanja huo wa ndege.

Touissant anasema kwamba Marekani na Ufaransa hawana madaraka ya kuamua ni nani ataongoza Ivory Coast. Anasema msaada wa nje anaopata Rais anayetambuliwa kimataifa Alassane Ouattara unachochea hali ya vurugu. Toussaint anasema Marekani na Ufaransa zimeshiriki kudumaza hali nchini Ivory Coast tangu uchaguzi wa marudio wa urais.

Wakati mapigano ya kutwaa mji wa Abidjan yakiingia siku ya tano, makundi ya haki za binadamu yametoa wito kwa majeshi yanayowatii Bw. Ouattara na Bw. Gbagbo kuheshimu haki za raia. Touissaint amekanusha ripoti kwamba wapiganaji wanaomuunga mkono rais anayeng’ang’ania madarakani wana orodha ya watu wanaokusudia kuua huko Abidjan.

Wapiganaji wanaomuunga mkono Outtara wamesonga kwa kasi katika sehemu kubwa ya nchi katika wiki moja iliyopita katika harakati zao kuelekea mji wa Abidjan, lakini hawamiliki eneo lote ambalo linaaminika kuwa ngome kuu ya wafuasi wa Bw. Gbagbo huko jimbo la kusini mashariki.

XS
SM
MD
LG