Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:25

Seneta maarufu wa Marekani John McCain aaga dunia


Aliyekuwa seneta wa Arizona, John McCain.
Aliyekuwa seneta wa Arizona, John McCain.

Seneta maarufu wa Marekani, John McCain, aliaga dunia Jumamosi akiwa na umri wa miaka 81.

McCain ambaye alikuwa anaugua saratani ya ubongo, alifariki katika chumba chake cha mapumziko mjini Sedona, Arizona, akiwa amezungukwa na familia yake.

Mwanasiasa huyo mkongwe aligunduliwa kuwa na ugonjwa huo hatari mnamo mwezi Julai mwaka 2017.

Famila ya McCain ilitangaza Ijumaa kwamba alikuwa amesitisha tiba "kwa sababu saratani imeenea sana."

Hadi kifo chake, McCain alikuwa anawakilisha jimbo la Arizona katika seneti ya Marekani.

Atakumbukwa kama mmoja wa mashujaa wa vita vya Vietnam na kati ya wanasiasa wachache walioshikilia misimamo yao kwa dhati bila kujali misingi ya vyama hata akapewa jina la utani "Maverick."

Alishikiliwa kwa miaka mitano kama mateka wa kivita nchini Vietnam kabla ya kurejea Marekani na kujitosa kwa siasa.

Alihudumu katika bunge la Marekani kwa miongo mitatu na aliwahi kuwa mgombea wa urais kwa tikiti ya chama cha Republican mara mbili.

Mnamo mwaka wa 1999, alimpinga rais wa wakati huo, George W Bush lakini akakosa kupata tikiti ya chama.

Alijitosa uwanjani tena mwaka wa 2007 na kuteuliwa kama mgombea rasmi mwaka wa chama cha Republican kwenye uchaguzi wa mwaka uliofuata ambapo alipambana na kushindwa na mgombea wa chama cha Demokratik, Barack Obama.

Punde tu baada ya habari za kifo chake kuchipuka Jumamosi, viongozi wa tabaka mbalimbali walianza kutuma jumbe za rambirambi hususan kupitia mitandao ya kijamii, wengi wakimtaja kama shujaa.

"Tumempoteza shujaa shupavu," aliandika aliyekuwa mgombea mwenza wa urais, Sarah Palin kwenye Twitter.

"Nilikuwa na baba yangu wakati aliaga dunia kama alivyokuwa nami wakati nilizaliwa," alisema mwanawe McCain, Meghan McCain katika ujumbe mrefu uliotumwa kwa vyumba vya habari.

Rais Trump aliandika kwenye Twitter: "Maombi yangu yaindee familia ya Seneta McCain."

Jumamosi jioni, bendera ya Marekani kwenye ikulu, White House, iliteremshwa nusu mlingoti kwa heshima ya mwanasiasa huyo.

Kati ya nyakati ambpo alishikilia msimamo wake pasina kujali chama, ni wakati aliporejea kwenye seneti kupiga kura muhimu mwaka jana ambayo ilinuia kubadilisha hatma ya mswada ulioungwa mkono na rais Trump kutaka kuibailisha kabisa sheria ya bima ya afya maarufu kama Obamacare.

Seneta McCain alipinga mswada huo na kusambaratisha juhudi za Rais Trump. Hadi wakati wa kifo cha McCain, Trump alikuwa akimlaumu kwa kufeli kwa mswada huo, ambao ulikuwa moja ya nyenzo muhimu wakati wa kampeni za urais za mwaka wa 2016.

McCain alizaliwa mwaka wa 1936 na aliwahi kuhudumu katika jeshi la wanamji kabla ya kuingia kwenye jeshi la wanahewa.

"Nimeishi maisha ya kuridhia na nina shukrani nyingi mno kwa yale niomeyatimiza katika maisha haya," alinukuliwa na vyombo kadhaa vya habari vya Marekani akisema, hususan alipoulizwa angependa kukumbukwa vipi.

McCain alizaliwa mwaka wa 1936 na aliwahi kuhudumu katika jeshi la wanamaji kama rubani.

Amemwacha mjane, watoto saba, mama yake na wajukuu watano.

XS
SM
MD
LG