Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 18:24

Rwanda : Mwanamuziki Kizito Mihigo ajinyonga akiwa chini ya ulinzi wa polisi


Kizito Mihigo
Kizito Mihigo

Jeshi la polisi nchini Rwanda linasema mwanamuziki mashuhuri wa muziki wa injili nchini Kizito Mihigo, 38, alikutwa amejinyonga alipokuwa yuko chini ya ulinzi katika kituo cha polisi mjini Kigali.

Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa mwanamuziki huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa alifariki majira ya saa za asubuhi.

Kizito alikuwa amekaa siku tatu kwenye kizuizi cha polisi baada ya kukamatwa kwenye kile polisi walichodai ni jaribio la kutorokea nchini Burundi kupitia upande wa kusini mwa nchi ili kujiunga na makundi yenye silaha.

Tangazo lililotolewa na polisi ya Rwanda limesema "Leo majira ya alfajiri saa kumi na moja Kizito Mihigo, 38, aliyekuwa akizuiliwa kwenye kituo cha polisi cha Remera mjini Kigali amekutwa amejinyonga na kufariki dunia."

Tangazo hilo liliendelea kusema kuwa Kizito alikuwa amemaliza "siku tatu akizuiliwa kwenye kituo hicho kwa shutuma za kosa la kujaribu kuvuuka mipaka ya nchi kinyume cha sheria pamoja na kujaribu kutoa rushwa."

Mwanamuziki huyu mara ya kwanza alikamatwa 2015 na kuhukumiwa kifungo cha miaka kumi jela baada ya kukutikana na hatia ya kushirikiana na makundi yenye silaha yaliyokuwa na nia ya kuipindua serikali ya Rwanda.

Lakini mwaka 2018 akaachiwa huru kwa msamaha wa Rais Paul Kagame akiwa pamoja na wafungwa wengine 2,140 - akiwemo mwanasiasa mpinzani wa serikali ya Rwanda mwanamama Victoire Ingabire kiongozi wa chama kilichopigwa marufuku nchini Rwanda cha FDU Inkingi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG