Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 04:37

Rwanda imeipiga ndege ya kivita ya DRC, Kinshasa imesema haitaendelea kuvumilia


Ndege kivita aina ya Sukhoi-25
Ndege kivita aina ya Sukhoi-25

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imeonya kwamba haitaendelea kuvumilia kile imekitaja kama unyanyasaji wa jirani yake Rwanda, licha ya kutakiwa kufuata utaratibu wa kuleta amani mashariki mwa nchi hiyo na kwamba ina haki ya kujilinda na kulinda ardhi yake kwa nguvu zote.

Hii ni baada ya ndege ya kijeshi ya DRC kupigwa kombora na wanajeshi wa Rwanda Jumanne jioni.

Serikali ya Rwanda imechapisha taarifa kwenye Twitter na kuthibitisha kuishambulia ndege ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo - DRC, ikidai kwamba ndege hiyo ilikuwa imeingia katika anga yake.

“Leo, saa kumi na moja na nusu jioni, ndege ya kivita aina ya Sukhoi-25 kutoka DRC iliingia katika anga ya Rwanda, hii ikiwa ni mara ya tatu,” imesema taarifa ya serikali ya Rwanda inayoeleza kwamba “hatua za kiulinzi zilichukuliwa" na kwamba "Rwanda inaitaka DRC kuacha uchokozi wa aina hii.”

Video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha kombora likiipiga ndege ya kivita kutoka nyuma.

Kombora la kwanza limekosa shabaha na kuipita ndege hiyo kabla ya kombora la pili kuipiga kutokea nyuma lakini haikuanguka.

VOA haijathibitisha uhalali wa video hiyo.

Kulingana na picha ambazo zimethibitishwa na mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika VOA, akiwa Goma, ndege hiyo imeharibika kwa kiwango kidogo sana, na ina matundu yanayoashiria kwamba ilipigwa pia risasi kadhaa.

Rubani wa ndege alifanikiwa kutua katika uwanja wa ndege wa Goma, DRC bila usumbufu mkubwa.

Ni vigumu kubaini anga ambayo ndege hiyo ilikuwa ikipaa kwa kutumia macho ya kawaida pasipo teknolojia ya anga au picha za satellite.

Video inaonyesha kwamba aliyerekodi alikuwa upande wa Rwanda kwenye mpaka wa Gisenyi na Goma.

Ni vigumu kwa mtu wa kawaida kutambua iwapo ndege hiyo ilikuwa Gisenyi au Goma.

Taarifa ya serikali ya DRC

Serikali ya DRC imelaani vikali shambulizi dhidi ya ndege yake na kusema kwamba ndege hiyo ilikuwa inajitayarisha kutua mjini Goma - DRC, na hakuna ishara kwamba ilikuwa inataka kutua Rwanda au ilikuwa katika anga ya Rwanda.

“Ndege hiyo ya mashambulizi ilishambuliwa wakati ilikuwa ianaanza kutua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma. Shambulio la Rwanda lilipelekea ndege ya Congo iliyokuwa inasafiri ndani ya mipaka ya Congo na wala haikuwa imevuka mpaka na kuingia katika anga za Rwanda, kuharibika kwa kiwango kidogo.” Imesema taarifa ya wizara ya habari na mawasiliano ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Taarifa ya serikali ya DRC inaendelea kusema kwamba “shambulizi hilo ni pamoja na shambulizi lililoanzishwa asubuhi ya leo (Januari 24, 2023) na jeshi la Rwanda kuelekea Kichanga na jeshi hilo kurudishwa nyuma mara moja na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo FARDC.”

DRC imedai kwamba wanajeshi wa Rwanda wamekuwa wakijitayarisha kuishambulia Congo.

“Katika kipindi hiki kumeshuhudiwa kundi la wanajeshi wa Rwanda wakitokea Rwanda ili kuimarisha vituo vyao vya Kibumba na Bwito kwa ajili ya vitendo vingine vya uhalifu.”

Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) na mwenzake wa Rwanda Paul kagame
Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) na mwenzake wa Rwanda Paul kagame

‘Uchokozi ndege za DRC kuingia Rwanda’

Mnamo Novemba 7, 2022, ndege ya kivita ya DRC iliripotiwa kuingia katika anga ya Rwanda na kutua katika uwanja wa ndege wa Rubavu, magharibi mwa Rwanda kwa dakika chache kabla ya kuondoka.

Rwanda ilitoa taarifa ikiitaja hatua hiyo kuwa ya kichokozi na ya kutaka kulichochea jeshi lake kuchukua hatua.

Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alisema mwezi Desemba mwaka uliopita kwamba “serikali ya DRC imeendelea kukiuka makubaliano ya amani ya Luanda, Angola na kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa inayoendelea kuilaumu Rwanda kwa matatizo na shida zilizoko DRC.”

Mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la DRC

Kuna taarifa kwamba ndege hiyo ilikuwa inatoka kufanya mashambulizi dhidi ya kundi la waasi la M23 ambalo limepelekea uhusiano kati ya DRC na Rwanda kuharibika.

Mapigano yamezuka tena mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha vita kati ya serikali na makundi ya waasi.

Mapigano kati ya jeshi la waasi wa M23 yameendelea Jumanne na kusababisha watu kadhaa kutoroka makwao.

Jeshi la serikali halijatoa taarifa yoyote kuhusu mapigano hayo lakini msemaji wa waasi wa M23 amewashutumu wanajeshi wa serikali kwa kile alichosema kwamba wameshambulia ngome zao walipokuwa wanajitayarisha kuondoka kama ilivyokubaliwa katika mazungumzo ya Luanda, Angola.

DRC inadai kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana vita na wanajeshi wa serikali mashariki mwa DRC.

Nchi za magharibi na wataalam wa Umoja wa Mataifa wamekubaliana na DRC kwamba kuna ushahidi wa kutosha kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23.

Rwanda imekana kabisa shutuma hizo na badala yake inadai kwamba DRC inawaunga mkono waasi wa FDLR wenye nia ya kuuangusha utawala wa rais Paul Kagame.

Ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa inasema kwamba nchi zote mbili zinayaunga mkono makundi ya waasi.

Rwanda inawaunga mkono M23 na DRC inawaunga mkono FDLR.

Waasi wa M23 wakiwa wameshika doria katika mji wa Kibumba mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Dec 23, 2022
Waasi wa M23 wakiwa wameshika doria katika mji wa Kibumba mashariki mwa jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Dec 23, 2022

Mchakato wa amani wa Luanda na Nairobi

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi alisisitiza wiki iliyopita akiwa Davos kwamba waasi wa M23 walikuwa hawajaondoka katika sehemu walizokuwa wanazishikilia na kwamba walikuwa wanajiimarisha katika sehemu nyingine za DRC licha ya kudai kwamba walikuwa wanaondoka.

Waasi wa M23 wamemshutumu Tshisekedi kwa kutaka "kuwaangamiza badala ya kusuluhisha vita hivyo kwa njia ya amani."

DRC imesema kwamba “inalichukulia shambulizi hilo baya la Rwanda dhidi ya ndege yake kama hatua ya kusudi ya uvamizi ambayo ni sawa na hatua ya vita ikiwa na lengo la kuvuruga juhudi zinazoendelea hivi sasa kuweka hatua zilizokubaliwa katika makubaliano ya Luanda na Nairobi kwa ajili ya kudumisha amani mashariki mwa DRC na kanda nzima ya Maziwa Makuu.”

Kinshasa inatoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua “hatua zinazohitajika na za dharura kuiwekea shinkizo Rwanda na kundi la kigaidi la M23 ili waache ghasia zinazohatarisha mchalatp wa uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2023” nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Umoja wa Mataifa umesema kwamba zaidi ya watu 400,000 wametoroka makwao kutokana na vita vinavyoendelea mshariki mwa DRC tangu mwaka uliopita, kati ya kundi la waasi la M23 na wanajeshi wa serikali ya DRC.

XS
SM
MD
LG