Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 14:48

Russia yahusishwa na shambulizi la kemikali lililofanywa na serikali ya Syria


Shambulizi la majeshi ya serikali ya Syria katika mji wa Douma ulioko mashariki ya mji wa Damascus, April 7,2018.
Shambulizi la majeshi ya serikali ya Syria katika mji wa Douma ulioko mashariki ya mji wa Damascus, April 7,2018.

Wanaharakati wa upinzani nchini Syria na waokoaji wamesema Jumapili kuwa gesi ya sumu iliyotumika kuwashambulia waasi wanaoshikilia mji ulio karibu na Damascus imewauwa sio chini ya watu 40, madai ambayo yamekanushwa na serikali ya Syria.

Madai ya shambulizi hilo katika mji wa Douma lilitokea Jumamosi jioni mara baada ya kuanza mashambulizi yaliyofanywa na majeshi ya serikali ya Syria baada ya kusita makubaliono yaliyofikiwa kusimamisha mapigano.

Ripoti hizo hazikuweza kuthibitishwa na chanzo kingine huru.

Marekani imeitaka Russia kuacha kuisaidia serikali ya Syria mara moja na “kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika juhudi zake za kuendelea kuepusha, mashambulizi ya kinyama ya kutumia silaha za kemikali.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Heather Nauert amesema katika tamko lake kuwa Marekani inaendelea kufuatilia kwa karibu ripoti ya April 7 ya madai mengine ya shambulizi la kutumia silaha za kemikali, mara hii ikilenga hospitali katika eneo la Douma, nchini Syria.

Tamko hilo limesema “Russia, ikiendelea kutoa msaada wake thabiti kwa utawala wa Syria, hatimaye itawajibika kwa mashambulizi haya ya kinyama, ambayo yanawalenga wananchi wengi wasiokuwa na hatia, na kuuwawa kwa jamii nyingi zilizokuwa hazina ulinzi zilizoko Syria zikishambuliwa kwa silaha la kemikali.”

Majeshi ya upande wa serikali ya Syria yalipiga hatua kuelekea mji wa Douma, Mashariki ya Ghouta, Aprili 7, 2018, baada ya vikosi vya serikali hiyo kuanza tena mashambulizi kushinikiza waasi kuondoka katika eneo hilo.

Serikali ya Syria ikisaidiwa na nguvu za kijeshi za Russia, imemwezesha Rais wa Syria Bashar al-Assad kuyatokomeza majeshi ya maadui zake takriban kutoka eneo lote la Ghouta.

Russia imekanusha ripoti hizo za shambulizi la kinyama la silaha za kemikali katika eneo la Douma nchini Syria, Shirika la habari la Interfax limeripoti Jumapili, likieleza kauli ya Wizara ya Ulinzi ya Russia.

“Tunakanusha moja kwa moja taarifa hizo,” Meja Jenerali Yuri Yevtushenko, mkuu wa kituo cha amani na usuluhishi cha Russia, amenukuliwa akisema.

“Sisi tunatangaza kuwa tuko tayari kutuma wataalamu wetu wa miale, kemikali na ulinzi wa silaha za kibaiolojia kukusanya habari, mara tu mji wa Douma utakapo kombolewa kutoka kwa wanamgambo. Hili litathibitisha jinsi madai haya yalivyokuwa ni ya uongo,” Yevtushenko alinukuliwa akisema.

XS
SM
MD
LG