Kamati ya uchunguzi ya Russia imesema katika taarifa kwamba mkuu wake Alexander Bastrykin aliamuru kuanzishwa kwa kesi ya uhalifu dhidi ya muigizaji wa filamu na michezo ya kuigiza Arthur Smolyaninov, ambaye aliondoka Russia baada ya vikosi vya Moscow kuivamia Ukraine na kukosoa mara kadhaa vita vya Russia dhidi ya Ukraine.
Kulingana na taarifa hiyo, Smolyaninov “ alitoa msururu wa taarifa dhidi ya Russia katika mahojiano na vyombo vya habari vya magharibi. Kamati hiyo ya uchunguzi haikufafanua ni vitendo gani alivyofanya Smolyaninov ambavyo ni kosa la uhalifu na mashtaka yapi itatangaza dhidi yake.
Mahojiano ya hivi karibuni ya Smolyaninov yalizusha hasira miongoni mwa wafuasi wa Kremlin. Muigizaji huyo aliliambia gazeti la Novaya Europe kuwa ikibidi aende kupigana katika vita vya Ukraine, atapigana upande wa Ukraine.