Russia itaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Mali kupitia njia za serikali shirika la habari la RIA lilimnukuu mwanadiplomasia mkuu wa Russia akisema Jumatatu siku chache baada ya Bamako kukataa kuwepo kwa mamluki wa Russia.
Ufaransa, Canada, na mataifa 13 ya Ulaya wiki iliyopita yaliilaani Moscow kuwezesha madai ya kutumwa kwa kandarasi binafsi wa kijeshi kutoka kundi la Wagner linaloungwa mkono na Russia hadi Mali mahala ambako serikali inapambana na waasi wa kiislam.
Serikali ya Mali siku ya Jumamosi ilikanusha uwepo wa mamluki wa Russia lakini ilisema wakufunzi wa Russia walikuwepo kama sehemu ya makubaliano ya pande mbili, kati ya Mali na Russia. Ndege ya mizigo iliwasilisha helikopta nne, silaha, na risasi kutoka Russia hadi Mali mwezi Oktoba sehemu ya kile ambacho serikali ya Mali ilisema ni makubaliano ya kibiashara na taifa la Russia.
RIA Jumatatu ilimnukuu Pytr Ilichev mkurugenzi wa idara katika wizara ya mambo ya nje ya Russia kwa mashirika ya kimataifa akisema katika mahojiano kwamba Bamako ina haki ya kushirikiana na washirika wowote inaowataka katika mapambano yake na wanamgambo.