Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 18:39

Russia: "madai ya kuvuruga uchaguzi wa Marekani hayana msingi"


Yevgenye Nikulin (29) wa Russia ambaye anashukiwa kufanya udukuzi kwenye malengo ya Marekani.
Yevgenye Nikulin (29) wa Russia ambaye anashukiwa kufanya udukuzi kwenye malengo ya Marekani.

Maamuzi yamefanywa kwa kukurupuka, hasira ambayo haiendi sambamba na weledi wa kazi unaolingana na huduma za kweli za upelelezi wa kiwango cha kimataifa.

Kremlin imeshutumu vikali kuwa taarifa za Marekani zinazodai kuwa iliingilia kati uchaguzi wa rais kumsaidia Donald Trump kushinda uongozi wa kipindi cha miaka minne katika ikulu ya White House hazina msingi wowote, ni madai ya idara za upelelezi zenye uwezo mdogo.

Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov amesema Jumatatu, "madai haya hayana msingi wowote ambapo hakuna usahidi wa kuyathibitisha, ikiwa yamefanywa kwa kukurupuka, hasira ambayo haiendi sambamba na weledi wa kazi unaolingana na huduma za kweli za kipelelezi zenye kiwango cha kimataifa."

"Tumechoshwa na kuongezeka kwa shutuma hizi," amesema Peskov, "imekuwa sasa ni kitendo cha kuendeleza kumtafuta mchawi."

Matamshi yake yalikuwa ni kauli ya kwanza kutolewa na Kremlin tangu idara za upelelezi za Marekani Ijumaa kusema kuwa ilikuwa na "imani kubwa" kwamba rais wa Russia, Vladimir Putin yeye mwenyewe aliamrisha kuanzishwa kwa kampeni za kuvuruga mchakato wa uchaguzi wa kidemokrasia wa rais nchini Marekani.

Maafisa wa Marekani wamesema juhudi za Russia zilielekezwa kuvuruga nafasi ya ushindi wa mgombea wa Demokratik, Hillary Clinton na kumsaidia Trump, ambaye ni mgombea wa Republikan.

Peskov amesema Russia inandelea "kukanusha kuhusika kwa namna yoyote" katika udukuzi wa maelfu ya barua pepe kutoka kwenye kompyuta ya mkuu wa kampeni ya Clinton, John Podesta na kuzisambaza nyaraka hizo kwa mtandao wa Wikileaks.

Kuendelea kusambazwa kwa barua pepe hizo mwezi mmoja kabla ya uchaguzi kumeonyesha wakati mwingine kuaibika kwa maafisa wa chama cha Demokratik katika juhudi zao za kumsaidia Clinton kumshinda seneta wa Vermont, Bernie Sanders katika kinyang'anyiro cha awali cha kupendekezwa kuwa mgombea urais katika tiketi ya chama chake.

"Mpaka hivi sasa hatujui ni takwimu gani zinazotumiwa na wale wanaoelekeza tuhuma zisizokuwa na msingi," msemaji wa Kremlin ameeleza.

Hivi karibuni Marekani ilitoa sehemu ya ripoti ya kipelelezi ambayo iliruhusiwa kusomwa na watu wote inayoelezea yale yaliyogundulika katika uchunguzi.Muhtasari huo wa kipelelezi ulikabidhiwa kwanza kwa rais Barack Obama siku ya Alhamisi na siku tatu baadaye alipelekewa rais mteule Trump.

Msemaji wa Kremlin amesema kuwa mara baada ya Trump kuapishwa huko Washington utaratibu utaanza wa kutafuta tarehe maalum ya kuandaa mkutano kati ya viongozi wa Marekani na Russia.

Mkuu wa wafanyakazi anayeingia madarakani aliyeteuliwa na Trump, Reince Priebus, amesema Jumapili kwamba rais mteule hajakanusha kuwepo kwa baadhi ya watu ambao walihusika katika uhalifu wa mitandao.

Lakini hivi karibuni Obama alisema, "nafikiri nilikuwa nimekadiria vibaya kiwango ambacho, katika zama hizi za teknolojia ya habari, ni rahisi kwa taarifa potofu kupenyezwa kwenye mitandao na mengineyo, kuwa na athari katika jamii zetu zilizokuwa na uwazi, mifumo yetu inayofikiwa, inawezekana maadui zetu kujipenyeza katika harakati zetu za kidemokrasia katika njia ambazo nafkiri zinazonekana kutia wasi wasi."

Amesema kuwa aliamuru kutolewa muhtasari wa taarifa za kipelelezi juu ya uhalifu wa mitandao uliofanywa na Russia, ili kuhakikisha tunalifahamu hili jambo ambalo Putin amekuwa akilifanya kwa muda mrefu hivi sasa huko Ulaya, mwanzoni katika yaliyokuwa majimbo katika himaya ya Umoja wa Sovieti ambako kuna watu wengi wanaozungumza kirusi, lakini hivi leo uingiliaji wake umezidi katika demokrasia ya nchi za magharibi.

XS
SM
MD
LG