Amesema hayo akiwa Kampala, Uganda katika ziara yake ya nchi nne
za Afrika.
Uganda ni nchi ya tatu kwenye ziara yake Afrika. Sergey Lavrov
ameendelea kusisitiza kwamba Russia haihusiki kwa vyovyote na
ukosefu wa nafaka, ngano, mafuta na kupanda kwa gharama ya maisha
kote duniani, kama inavyoripotiwa kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine.
Lavrov amedai kwamba mataifa ya Magharibi yamekuwa na hulka ya
kuilaumu Russia kwa kila baya, akisema kwamba gharama ya maisha
ilianza kupanda kabla ya vita vya Ukraine, kwanza kutokana na janga la
virusi vya Corona.
Licha ya kudai kwamba Russia haihusiki na hali mbaya ya uchumi
duniani, amedai kwamba vikwazo vya mataifa ya Magharibi dhidi ya
Russia ndiyo vimechangia hali hiyo, kwa kuvuruga usafirishaji wa
bidhaa muhimu.
Mafuta kwa Uganda kutoka Russia
Amesema kwamba Russia ipo tayari kuiuzia Uganda mafuta kwa bei
rahisi.
“Tunauza mafuta kwa nchi ambazo zipo tayari kushirikiana nasi. Kama
kuna nchi inataka kununua mafuta yetu, iwe India au Afrika, hatuna
kizuizi chochote.” Amesema Lavrov, akiongezea kwamba “siyo tu
kwamba tunauza mafuta, lakini pia tunatoa msaada katika sekta nyingine za maendeleo katika sekta ya mafuta. Tupo tayari vile vile kufanya mazungumzo na Uganda kuhusu swala hili.”
Russia ilikuwa inauza mapipa milioni 2.5 ya mafuta kila siku kabla ya
kuwekewa vikwazo kutokana na vita dhidi ya Ukraine kuanza.
Kufikia sasa, Mafuta ya dizeli kutoka Russia kuelekea Afrika imefikia
tani milioni 1 tangu kuanza kwa mwaka huu. Kiasi kikubwa cha mafuta
hayo kinaingia Senegal na Togo.
Museveni anataka maelezo kuhusu usafirishaji wa nafaka
Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amesema kwamba anataka
maelezo kutoka kwa Lavrov sababu zinazopelekea nafaka na mbolea
kutofika soko la kimataifa kutoka Russia na Ukraine licha ya kwamba
havijawekewa vikwazo.
Amesema kwamba maelezo ya Lavrov ni kwamba mataifa ya Magharibi
yamezuia meli za Russia kuingia katika bandari kadhaa duniani na hivyo
bidhaa hizo haziwezi kusafirishwa.
“Ameniambia kwamba mataifa ya Magharibi yamezuia meli za Russia
kusafirisha nafaka katika bandari mbalimbali duniani kwasababu ya
vikwazo.” Amesema rais wa Uganda Yoweri Museveni.
Tani milioni 22 za ngano zimekwama katika bandari za Ukraine tangu
kuanza kwa vita vya Ukraine.
Russia iliishambulia bandari kwa mabomu baada ya kusaini mkataba wa
kusafirisha nafaka
Russia na Ukraine zilisaini makubaliano ya kusafirisha nafaka baada ya
mazungumzo yaliyoongozwa na Uturuki Pamoja na umoja wa mataifa.
Hata hivyo Russia ilishambulia bandari ya Odessa, saa chache baada ya mkataba kusainiwa.
Uganda inasisitiza kwamba haitajiingiza katika mgogoro kati ya Russia na Ukraine, na kwamba Russia imekuwa Rafiki wa mda mrefu na itaendelea na ushirika wao kwa kila hali licha ya vikwazo vya nchi za magharibi.
Umoja wa ulaya unasema ziara ya Lavrov ni ya kueneza uongo
Balozi wa Umoja wa ulaya nchini Marekani Stavros Lambrinidis, anasema kwamba ziara ya Sergei Lavrov Afrika ni ya kueneza propaganda na uongo baada ya kujua vizuri kwamba uvamizi wa Russia nchiniUkraine unaendelea kuathiri duniani kwa jumla.
Katika mahojiano na Sauti ya Amerika, Lambrinidis amesema kwamba Russia inaendelea kuvuga kanuni zote za amani duniani, na ni lazima iwajibishwe na kuheshimu sheria ya kimataifa.
Mataifa ya magharibi yanasisitiza kwamba vikwazo dhidi ya Russia vimeanza kuiumiza nchi hiyo na hivyo Lavrov anatafuta soko kwa bidhaa zake.
Lavrov anatarajiwa mjini Addis Ababa, Ethiopia, makao makuu ya umoja wa Afrika, ambapo wachambuzi wa siasa za Afrika wanasema kwamba ziara yake nchini Ethiopia ni ishara kwamba ametembelea nchi zote za Afrika kabla ya kuwa mwenyeji wa kongamano la viongozi wa Afrika mjini Moscow, mwaka ujao.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC