Rais wa zamani wa muda mrefu nchini Zimbabwe Robert Mugabe amefariki akiwa na umri wa miaka 95. Rais wa Zimbabwe Emerson Mnangagwa alitangaza kifo cha Mugabe kupitia ukurasa wake wa Twitter, akimtaja Mugabe baba wa taifa kama shujaa wa ukombozi na mtetezi wa maslahi ya Afrika katika kipindi cha uhai wake.
Mugabe aliingia madarakani wakati wa uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980 baada ya vita vya msituni vilipomaliza utawala wa wazungu walio wachache wakati taifa hilo likifahamika kama Rhodesia.
Alionekana kiongozi wa kuigwa barani Afrika pale alipochukua madaraka lakini taswira hiyo ilitoweka mwishoni mwa utawala wake pale utawala huo ulipogeuka na kuwa wa kimabavu.
Robert Mugabe alizaliwa Februari 21 mwaka 1924 huko Zvimba kusini magharibi mwa mji mkuu wa Zimbabwe wakati huo ukiitwa Salisbury na hivi sasa unajulikana kama Harare.