Rais Xi Jinping wa China alitetea mradi wa kisera katika ufunguzi wa kongamano la Belt and Road Initiative mjini Beijing akiangazia kile anachosema ni mafanikio ya mpango huo katika muongo mmoja uliopita.
Huku Rais wa Russia Vladimir Putin akiwa mgeni mashuhuri kati ya waliohudhuria mkutano huo na akiwa kando yake, pia alielezea maeneo manane muhimu ambayo China inalenga kuimarisha maendeleo.
Jukwaa hilo ambalo lilianzishwa ili kukuza muunganisho wa kimataifa lakini lilijumuisha wakuu wa nchi wachache kuliko mikutano ya awali, linakuja wakati dunia inazidi kusambaratika kutokana na vita nchini Ukraine na hali ya wasiwasi ikiongezeka huko Mashariki ya Kati.
Baadhi ya wachambuzi wanasema Beijing inataka kongamano hilo liimarishe hisia kuwa China ni kiongozi wa dunai inayoendelea.
BRI imekuwa ajenda ya sera ya mambo ya nje ya China, na mtizamo ambao Beijing imewasilisha kupitia mpango huo ni kwamba China inachangia maendeleo ya miundo mbinu na uchumi kwa dunia inayoendelea, Yun Sun, mkurugenzi wa programu ya China katika Kituo cha Stimson, kituo cha wataalam chenye makao yake mjini Washington D.C. aliiambia VOA
Viongozi na wawakilishi kutoka nchi 140, wengi wao kutoka Ukanda wa Kusini duniani walihudhuria mkutano huo wa siku mbili, akiwemo Putin wa Russia ambaye alifanya mkutano wa ana kwa ana na Xi pembeni ya kongamano hilo.
Ni tukio kubwa la kwanza la kimataifa ambalo China imelifanya tangu ilipoibuka kutoka kwenye kizuizi cha janga la covid takriban miaka mitatu hapo Januari 2023.
Akipongeza mafanikio ya BRI tangu mwaka 2013, Xi alisema mpango huo umesaidia kutatua matatizo ya nishati na kufungua njia mpya za kiuchumi kwa nchi nyingi zinazoendelea, wakati bandari, barabara na reli zilizojengwa chini ya BRI zimeruhusu bidhaa, fedha, teknolojia na watu kuzunguka kati ya mabara.
Forum