Katika kauli zake mjini Kinshasa alikoanzia na kisha kuelekea Bukavu, Hollande alionyesha nia ya kuona mipango ya kidiplomasia iliyoanzishwa hivi karibuni na Ufaransa katika ukanda wa maziwa makuu katika kukomesha uingiliaji wa nje, inatekelezwa.
Kiongozi huyo amesema anaamini kwamba kufikia sasa muungano wa vikosi vya ujumbe wa Umoja wa mataifa nchini Congo, Monusco, pamoja na vifaa vyao, si kamilifu na kwa hivyo angependa viimarishwe, ili vifanye kazi kama inavyo stahili, katika kupambana na makundi yenye silaha.
Jumatano, Hollande akiandamana na mkewe Julie Gayet, pamoja daktari mashuhuri Denis Mukwege, walizindua jengo la huduma mpya ya upasuaji katika hospitali yake ya Panzi.
Wakati huo huo, wahanga wa dhuluma za ngono na ubakaji wanaopokea matibabu katika hospitali hiyo, walipata fursa ya kueleza masaibu yao kwa Hollande.
Hayo yanajiri wakati baadhi ya asasi za kiraia zinapanga kufanya maandamano Alhamisi, mjini Bukavu kudai ukombozi wa mji mdogo wa Bunagana kutoka mikononi mwa waasi wa M23.