Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 15:01

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya afariki kutokana na Covid-19


Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya
Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya

Aliyekuwa rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya, amefariki dunia usiku wa jana kuamkia ijumaa hii akiwa na umri wa miaka 71 kutokana  na ugonjwa wa Covid 19, vyanzo mbalimbali vya habari vimesema.

Taarifa zinasema Buyoya alipatwa na virusi vya corona akiwa mjini Bamako nchini Mali. Alilazwa hospitalini kwa wiki moja mjini humo akipewa huduma za afya.

Lakini hali yake ya afya ilikuwa mbaya ghafla na akasafirishwa kwa ndege yenye matibabu mjini Paris usiku wa Alhamisi lakini alifariki dunia baada tu ya kuwasili nchini Ufaransa kabla ya kufikishwa hospitali.

Wiki tatu zilizopita, Buyoya alijiuzulu kwenye wadhifa wake kama mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini Mali na katika kanda ya Sahel, akisema alifanya hivyo ili aandae utetezi wake katika kesi ya mauaji ya mtangulizi wake Melchior Ndadaye iliyokua inamkabili.

Alijiuzulu kwenye wadhifa huo ambao alikuwa anashikilia tangu mwaka wa 2012 baada ya kuhukumiwa na mahakama ya juu ya Burundi kifungo cha maisha jela, katika kesi ilioendeshwa bila yeye mwenyewe kuwepo.

Buyoya alikanusha shutuma dhidi yake, akisema kesi hiyo imechochewa na sababu za kisiasa.

Buyoya aliiongoza Burundi mara mbili: kuanzia mwaka wa 1987 hadi 1993, alipokabidhi madaraka kwa rais wa kwanza kutoka Kabila la Wahutu Melchior Ndadaye, ambaye alimshinda kwenye uchaguzi.

Ndadaye aliuawa katika mapinduzi ya kijeshi baada ya kuongoza kwa miezi mitatu.

Buyoya alirudi tena madarakani mwaka wa 1996 katika mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Sylvestre Ntibantunganya, na kuongoza hadi mwaka wa 2003.

Alikuwa kiongozi wa mpito wa muungano wa kitaifa, kufuatia makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Arusha, Tanzania mwaka wa 2000 na pande zilizokuwa zinazozana, ili kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya muongo mmoja vilivyosababisha vifo vya takriban watu laki 3.

-Imetayarishwa na Patrick Nduwimana, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG