Matarajio yalionyesha Macron atashinda kwa kati ya asilimia 28 na 29 huku Le Pen akiwa na kati ya asilimia 23 na 24. Wakiwa washindi wawili wa juu, wanaosonga mbele kwenye duru ya pili ya uchaguzi tarehe 24 April.
Rais Macron amewataka wafuasi wake kutolegeza kamba kwani bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili wapate ushindi kwenye duru ya pili.
“Katika siku 15 zijazo, tuongeze juhudi kwa sababu kazi haijakamilika. Tuwe wanyenyekevu, tuwe na dhamira. Twende tukamshawishi kila mtu, tarehe 24 Aprili, tunaweza kuchagua enzi mpya ya Ufaransa na Ulaya,” Macron amesema.
Mgombea wa mrengo mkali wa kushoto Jean Louis Melanchon ameshika nafasi ya tatu na kura zinazokadiriwa kuwa kati ya asilimia 20 na 21.
Naye mwanasiasa wa mrengo mkali wa kulia Eric Zemmour, ambaye amegombea kwa mara ya kwanza, anatarajiwa kupata kati ya asilimia 6.5 na asilimia 7.1.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa leo Jumatatu asubuhi.