Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 11:56

Rais wa Malawi anaanza siku 21 za kufunga na maombi kusitisha Corona nchini humo


Rais wa Malawi Lazarus Chakwera akiwa Lilongwe, Malawi, June 28, 2020.
Rais wa Malawi Lazarus Chakwera akiwa Lilongwe, Malawi, June 28, 2020.

Chakwera alisema ongezeko la maambukizi ni kubwa Malawi kwa sababu watu wengi akiwemo yeye mwenyewe walipuuzia masharti ya wataalam wa afya ya kujikinga na COVID-19 ikiwemo kuvaa barakoa

Rais wa Malawi Lazarus Chakwera anasema amehuzunishwa na takwimu zinazoonesha ongezeko la karibuni la maambukizi ya virusi vya Corona nchini mwake. Katika hotuba ya Jumapili kwa njia ya redio alitangaza anaanza siku 21 za kufunga na kumuomba mungu aepushe janga ambalo limeongezeka tena. Wataalamu wa afya wanasema hali iliyopo nchini humo inahitaji zaidi ya maombi ya sala.

Malawi hivi karibuni imeshuhudia ongezeko katika kesi za virusi vya Corona. Tangu Alhamis nchi hiyo imekuwa ikithibitisha kesi nyingi za COVID kuwahi kurekodiwa.

Kwa mfano Jumamosi, Malawi ilirekodi kesi 381 za virusi vya Corona na vifo 12 idadi kubwa sana kwa siku moja tangu iliporekodi kesi zake tatu za kwanza hapo April mwaka jana.

Chakwera alisema ongezeko la maambukizi ni kubwa kwa sababu watu wengi akiwemo yeye mwenyewe walipuuzia masharti ya kujikinga na COVID-19.“Wengi wetu hatukuwa makini sana dhidi ya virusi hivi na sasa tunalipa gharama ya upuuzaji huo. Tunalipa gharama kwa sababu wengi wetu tumerudi kwenye hali ya zamani ya kutovaa barakoa, kutofuata masharti ya kutokaribiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine, na kuto-osha mikono kwa sabuni mara kwa mara. Ninaposema wengi wetu, ni pamoja na mimi mwenyewe”

Lazarus Chakwera , Rais wa Malawi
Lazarus Chakwera , Rais wa Malawi

Rais Chakwera mara kadhaa amekuwa akikosolewa kwa kupuuzia masharti ya kujikinga na COVID anapokuwa kwenye mikutano. Mwezi Oktoba mwaka jana Rais Chakwera alikabiliwa na ukosoaji wa umma kwa kutovaa barakoa, wakati alipokutana na kiongozi mwenzake wa Tanzania, John Magufuli, katika ziara ya kiserikali ya siku tatu kuitembelea Tanzania.

Mwezi Januari pia Chakwera alikosolewa baada ya kuonekana bila ya barakoa na kisha kupeana mikono na mwanamuziki wa kimarekani, Madonna alipomtembelea kwenye makazi yake, katika mji mkuu Lilongwe. Madona ana Watoto wanne wa kuasili kutoka Malawi na pia ni mwanzilishi mwenza wa taasisi moja ya hisani nchini humo.

Lakini katika hotuba yake ya Jumapili kwenye radio Chakwera alisema hivi sasa ni wakati kwa kila mtu nchini humo kurudia utekelezaji wa masharti ya kuzuia COVID-19.

“Kasi ambayo virusi vimekuwa vikienea tangu Krismas inasumbua sana. Maambukizi mapya 66 yalithibitishwa kati ya siku ya Krismasi na siku inayofuata yaani Boxing Day. Na katika wiki mbili zilizopita tangu hapo, zaidi ya maambukizi mapya 1,500 yamethibitishwa ambayo ni wastani wa maambukizi mapya zaidi ya 120 kila siku, ambayo yanaweka shinikizo kubwa katika mfumo wetu wa afya na wafanyakazi wa afya: hali hii haiwezi kuruhusiwa kuendelea”

Chakwera alisema ameziagiza wizara za usalama wa ndani na afya kuongeza utekelezaji wa miongozo ya kujikinga na COVID-19 mara moja. COVID-19 ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona.

Wizara ya afya nchini Malawi inasema kiasi cha watu 500 waliorudi kutoka Afrika kusini siku ya Jumamosi wametengwa katika kituo kimoja huko Blantyre kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya COVID-19.

XS
SM
MD
LG