Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 07:01

Rais Yoweri Museveni kusimamia mazungumzo ya kuleta amani Ethiopia


FILE PHOTO: Rais ya Uganda Yoweri Museveni alipohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na kwenye Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, Jan. 28, 2018.
FILE PHOTO: Rais ya Uganda Yoweri Museveni alipohudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika na kwenye Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia, Jan. 28, 2018.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni atasimamia mazungumzo ya kuleta amani nchini Ethiopia kati ya serikali na maafisa wa eneo la Tigray.

Kulingana shirika la habari la AFP, maafisa wa serikali ya Ethiopia wasiotaka kutajwa wamesema kwamba mazungumzo hayo yamepangwa kuanza Jumatatu, kaskazini mwa Uganda.

Naibu waziri mkuu wa Ethiopia Demeke Mekonnen Hassen, ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje, pamoja na wawakilishi wa Tigray, wanatarajiwa nchini Uganda Jumatatu kwa mazungumzo hayo.

Hayo yanajiri wakati kiongozi wa eneo lililojitenga nchini Ethiopia, Tigray, amethibitisha kwamba wapiganaji wake walifanya mashambulizi ya roketi kwenye uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Eritrea.

Shambulizi hilo linaongeza wasiwasi wa kusambaa kwa vita katika eneo hilo la pembe ya Afrika.

Debretsion Gebremichael, amesema kwamba wapiganaji wake walishambuliwa kila upande na maelfu ya wanajeshi wa Eritrea na vifaru anavyodai waliingia Tigray kuwasaidia wanajeshi wa Ethiopia.

Wanadiplomasia waliwaambia waandishi wa habari Jumamosi usiku kuwa makombora mengi yalipiga Asmara, yakitua karibu na uwanja wa ndege, ingawa vizuizi vya mawasiliano huko Tigray na Eritrea vilifanya ripoti hizo vigumu kuthibitisha.

Waziri mkuu Abiy Ahmed ameandika ujumbe wa Twitter kwamba Ethiopia ina uwezo wa kutosha kufanikisha malengo yake katika eneo la Tigray bila msaada wowote lakini hakujibu moja kwa moja madai ya Debretsion.

Mwanadiplomasia mkuu wa wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa Afrika, Tibor Nagy, alishutumu mashambulizi ya vikosi vya Tigray dhidi ya Eritrea na kulaani kile alichokiita juhudi zao za kuufanya mzozo huo kuwa wa kimataifa.

Abiy alizindua kampeni hiyo huko Tigray mnamo Novemba 4 baada ya kushutumu vikosi vya eneo hilo kwa kushambulia wanajeshi wa serikali kuu walio katika jimbo la kaskazini, ambalo linapakana na Eritrea na Sudan na lina makazi ya watu wapatao milioni 5.

Idadi ya watu ambao wamekimbilia Sudan kutokana na mzozo huo kaskazini mwa Ethiopia imeongezeka hadi 20,000, shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa na maafisa wa eneo hilo walisema Jumapili.

XS
SM
MD
LG