Rais Idriss Deby wa Chad siku ya Jumapili alitangaza hali ya dharura kitaifa katika majimbo mawili ya mashariki nchini humo baada ya mapambano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyosababisha darzeni ya vifo mwanzoni mwa mwezi huu.
Taarifa kutoka ofisi ya rais ilieleza kuwa hali ya dharura kitaifa itakuwepo kwa muda wa miezi mitatu katika maeneo ya Sila na Ouaddai mahala ambapo watu 50 wamekufa tangu Agosti 9 katika mapigano kati ya wafugaji na wakulima.
Rais Deby alieleza akiwa safarini kuelekea Sila kwamba serikali yake itapeleka vikosi vya jeshi ambavyo vinakwenda kuhakikisha usalama wa watu katika eneo hilo. Pia alisema lazima raia wote watue silaha zao chini.
Mashariki mwa Chad ni eneo lililopo kwenye mzunguko wa ghasia kati ya wafugaji ambao wengi ni kutoka kundi la kabila la Zaghawa mahala ambapo Deby anatokea na baadhi ya wakulima wanatoka jamii ya Ouaddian. Ukame na ongezeko la watu vimechangia mzozo kwenye eneo hilo pamoja na mmiminiko wa silaha holela kutoka maeneo jirani yenye mzozo kwa jumla vimechangia vifo kuongezeka.