Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 15:14

Raila Odinga: Haya ndiyo makubwa nitakayofanya nikiwa rais wa 5 wa Kenya


Mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga akiwa katika mahojiano na vyombo vya habari, Nairobi, Kenya. PICHA: REUTERS
Mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga akiwa katika mahojiano na vyombo vya habari, Nairobi, Kenya. PICHA: REUTERS

Mgombea wa Urais nchini Kenya Raila Odinga, ameahidi wakenya maisha mema ambayo kila mkenya atafurahia katika utawala wake endapo atashinda uchaguzi mkuu wa Agosti 9 2022.

Odinga, ambaye ni mwanawe makamu wa rais wa kwanza wa Kenya Jaramogi Oginga Odinga, anagombea urais katika jaribio lake la tano baada ya kufanya hivyo mwaka 1997, 2007 2013 na 2017 bila mafanikio.

Anagombea urais mwaka huu 2022 kupitia kwa muungano vyama vingi vya kisiasa, uliopewa jina Azimio la umoja.

Shabaha kuu katika manifesto ya Raila Odinga ni kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuleta mabadiliko ya kijamii na utawala bora.

Anaahidi wakenya kwamba ataangazia zaidi namna ya kupunguza gharama ya maisha, kuimarisha huduma ya afya, kubuni nafasi za kazi kwa kila mkenya, kuhakikisha kila boma lina maji safi, kupambana na ufisadi pamoja na kupambana na uhaba wa chakula.

Odinga, mwenye umri wa miaka 77, analenga kubuni sera zitakazohakikisha kwamba gharama ya maisha inashuka marudufu, katika mda wa siku 100 baada ya kuingia madarakani.

Gharama ya maisha, elimu bila malipo hadi chuo kikuu.

Kulingana na manifesto ya Raila Odinga, ambayo anafanya kampeni kwa kutumia maneno ‘inawezekana’, atapunguza gharama ya maisha ndani ya siku 100 kwa kupunguza bei ya mafuta ya petroli, bei ya unga, bei ya internet na nshati.

Walimu wote ambao wamehitimu na hawajapata kazi wataajiriwa punde tu anapoingia madarakani ili kuhakikisha kwamba elimu inayotolewa ni ya kiwango cha juu. Zaidi ya hilo, ameahidi wakenya kwamba serikali yake itatoa elimu ya bure kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu.

Kwa kuzingatia kwamba Utalii ni mojawapo ya sekta muhimu kwa uchumi wa Kenya, serikali ya Odinga itawafunga maisha gerezani wawindaji haramu na watu wanaofanya biashara ya pembe za ndovu na vitu vyote vinavyotokana na uwindaji haramu.

“Tutaanza kwa kuwekeza katika vifaa vya kisasa katika mbuga za wanyama za kitaifa ili kuwanasa wawindaji haramu. Tutawekeza zaidi katika utafiti namna ya kulinda mali zetu asili.” Amesema Odinga wakati wa uzinduzi wa manifesto yake hivi karibuni jijini Nairobi.

Wanajeshi kuongezewa mshahara

Manifesto ya Odinga inawaahidi wanajeshi wote wa Kenya nyongeza ya mshahara na kuboresha mazingira yao ya kazi katika mda wa siku 100 baada ya kuapishwa.

Mabadiliko yatafanyika katika idhara ya polisi ikiwemo kuwawezesha polisi kutumia mfumo wa kisasa wa kupambana na uhalifu na kuboresha zaidi kazi yao.

“Tutaweka polisi maalum sita kwa kila kituo cha polisi ili kushughulikia maswala ya vijana. Hili litaboresha uhusiano kati ya polisi na vijana. Tutaboresha mazingira ya kazi ya maafisa wa jeshi.”

Ufisadi

Ili kupambana vilivyo na ufisadi, kero ambalo wakenya wengi wanasema ndilo tatizo kubwa nchini humo, Odinga ameahidi kwamba kila mtu atakayehudumu katika serikali yake atasaidi mkataba unaomzuia kujihusisha na ufisadi. Hili litafanyika ndani ya siku 100 za utawala wake.

Kila afisa katika serikali yake, atahitajika kumchunguza mwingine na kuripoti vitendo vyovyote vya ufisadi katika idhara yake.

Odinga anapanga kuweka mikakati kuhakikisha kwamba watakaochaguliwa au kuteuliwa katika serikali yake hawataruhusiwa kujihusisha na biashara yoyote na serikali.

Ataagiza bunge kutunga sheria au kuweka kanuni zitakazohakikisha kwamba madai yote ya ufisadi yanachunguzwa kwa haraka, kesi kusikilizwa na kuamuliwa kwa haraka iwezekanavyo.

Isitoshe, ametangaza kwamba serikali yake itauchukulia ufisadi kuwa tishio kwa usalama wa nchi na kuunda idara maalum ya vyombo vya usalama vinavyohusika na ufuatiliaji wa ufisadi na kwamba maafisa wote wa serikali watahitajika kutangaza utajiri wao. Aidha, amesisitiza kuwa hatakubali tamaa, ulafi na ufisadi ulemaze maendeleo ya nchi kuendeleza maslahi ya kibinafsi ya watu wachache, akikariri kuwa maafisa wa serikali hawatapata kandarasi za serikali.

Bima ya afya - Baba care

Wahudumu wa afya wataajiriwa mashinani na kuwaezesha kufanikisha utoaji wa afya kwa wakenya.

Wafanyakazi wanaostaafu wataendelea kupata bima ya afya kwa gharama ya serikali. Bima ya afya ya Raila Odinga, ambayo itatolewa kwa kila Mkenya, itaitwa Baba care.

Ahadi kuu 10 za Raila Odinga kwa wakenya

  • Shilingi 6000 kwa kila familia maskini ili kukabiliana na ugumu wa maisha. Amesema mpango huu utaitwa ‘Inua jamii, pesa mfukoni’.
  • Bima ya afya kwa wakenya wote kote nchini – baba care
  • Kila boma lina maji safi bila upungufu wowote
  • Elimu bila malipo kutoka shule ya msingi hadi chuo kikuu
  • Kubuni nafasi za kazi kwa wakenya wote hasa kupitia uwekezaji katika sekta ya jua kali na miradi mingine midogo midogo
  • Kuhakikisha kuna chakula cha kutosha kote Kenya
  • Kufadhili biashara zinazomilikiwa na akina mama na kuhakikisha kwamba wanawake wanaakilishwa vikamilifu serikalini
  • Mafunzo ya kiufundi ili kuwawezesha vijana kubuni nafasi za kazi
  • Kila kaunti (47) ina kiwanda cha kuzalisha bidhaa.
  • Kuendeleza na kumaliza miradi iliyoanzishwa na rais Uhuru Kenyatta pamoja nna miradi ya serikali zilizotangulia.

Shilingi 6000 kila mwezi kwa familia maskini

Mpango utakaoitwa Inua Jamii, utawanufaisha watu kutoka jamii maskini, ambapo watapokea shilingi 6000 kila mwezi kutoka kwa serikali.

“Tutaanza mpango huu kwa kuwasaidia akina mama wanaolea watoto pekee yao, kubuni nafasi za kazi za mda kwa vijana, maarufu kazi mtaani .” ameahidi Odinga.

Katika serikali ya Raila Odinga, kila kaunti itakuwa na kiwanda cha kuzalisha bidhaa. Mpango huo anapanga kuuzindua ndani ya siku 100 za utawala wake endapo ataingia madarakani. Kenya ina kaunti 47. Viwanda vitakavyoanzishwa na vijana havitahitajika kulipa ada za leseni na mahitaji mengine ya serikali.

“Tutashirikiana na nchi zingine katika kuimarisha teknolojia yetu na kuhakikisha kwamba sera ya kununua bidhaa zinazotengenezwa Kenya ili kujenga Kenya, itatekelezwa vikamilifu. Wakenya wanaoishi ughaibuni na waekezaji kutoka nchi za nje, watapewa fursa nzuri na kusaidiwa na serikali kuekeza nchini Kenya.”

Odinga ameahidi kuwa sera ya serikali yake itaboresha kanuni za ushuru, fedha na kanuni nyinginezo kusaidia sekta hiyo pamoja na kubuni sera mpya ya utengenezaji wa bidhaa ili kukuza maendeleo ya raia wa Kenya na kuwa kichangiaji cha asilimia 30% kwa mapato ya taifa.

Kupambana na uhaba wa chakula

Kila mwaka, uhaba wa chakula huripotiwa nchini Kenya hasa sehemu za kaskazini mwa Kenya ambazokwa kawaida hazipokei mvua ya kutosha. Hivi sasa, Kenya inakabiliwa na uhaba wa chakula cha kutosha, bei ya unga ambao ni muhimu sana nchini humo kwa ajili ya kutengeneza ugali, ikiwa imepanda zaidi.

Serikali tayari imetangaza kwamba wafanyabiashara wataruhusiwa kuagiza mahindi kutoka nje ya nje na kutengeneza unga kwa haraka ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Katika Ajenda ya Fukuza Njaa, Odinga ameahidi kujitolea kwa serikali yake kuweka mazingira wezeshi kwa kilimo kinachozingatia hali ya hewa, usindikaji wa mazao ya kilimo, ufugaji bora wa mifugo na ukuaji wa uchumi utokanao na bahari, urekebishaji na upunguzaji wa mabadiliko ya hali ya anga ili kuwezesha na kunawiri kufikia tija ya juu ya kilimo kote nchini.

Ofisi maalum kwa ajili ya madeni ya serikali

Deni la Kenya limekuwa likiongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Serikali inalazimika kutenga kiasi kikubwa cha pesa katika bajeti yake kwa ajili ya kulipa madeni. Kenya, imekopa kiasi kikubwa cha pesa kutoka kwa nchi mbali mbali, mkopeshaji mkubwa akiwa ni serikali ya China.

Licha ya deni kubwa, Kenya inaendelea kukopa kila mwaka. Kwa sababu hiyo, utawala wa Odinga, umeahidi kuunda ofisi maalum kusimamia deni la taifa, kupunguza ukopaji usiokuwa wa lazima na badala yake kutumia makusanyo ya ushuru ya ndani kuendeleza miradi ya serikali.

Swala kuu ambalo Raila Odinga amekuwa akiahidi kila mwaka ni namna ya kuleta maridhiano ya taifa.

Na ilivyo na muungano wa vyama vya kisiasa anavyotumia mwaka huu kugombea urais, Azimio la umoja, ofisi maalum itaundwa kwa ajili ya waathiriwa wa mauaji ya watu katika mazingira ya kutatanisha, mateso, kuchunguza visa vya watu kutoweka katika hali isiyoeleweka. Ofisi hiyo itakuwa na jukumu la kuishauri serikali kuhusu hatua zinazostahili kuchukuliwa.

Raila Kuwa rais wa 5 wa Kenya?

Raila anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa naibu wa rais wa sasa William Ruto, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti 9 2022. wagombea wengine ni David Mwaure na Prof George Wajackoya.

Iwapo Raila Odinga atashinda uchaguzi wa urais, atakuwa kiongozi mwenye umri wa juu zaidi (77) kugombea nafasi hiyo na kushinda katika historia ya Kenya. Pia, atakuwa kiongozi ambaye amewahi kugombea mara zaidi ya 4 kiti cha urais nchini Kenya na kushindwa, kabla ya kushinda mara ya 5. Katika mikutano yake ya kisiasa, Odinga amekuwa akiwaambia wafuasi wake kwamba inawezekana.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC, akishirikiana na Kennedy Wandera, Nairobi.

XS
SM
MD
LG