Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Novemba 24, 2024 Local time: 13:06

Raila akataa matokeo ya uchaguzi wa rais Kenya


Aliyekuwa mgombea urais nchini Kenya, Raila Odinga.
Aliyekuwa mgombea urais nchini Kenya, Raila Odinga.

Aliyekuwa mgombea urais nchini Kenya, Raila Odinga, amesema kwamba hakubaliani na matokeo ya uchaguzi wa urais  yaliyotangazwa Jumatatu na Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini humo IEBC, na kwamba atachukua hatua zilizoainishwa kikatiba kuyapinga matokeo hayo.

Odinga alikuwa akizungumza katika ukumbi wa jengo la KICC Jumanne akiandamana na viongozi wenzake wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, akiwemo aliyekuwa mgombea mwenza wake, Martha Karua.

"Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, Wafula Chebukati hakuwashirikisha makamishna wote na tunayakataa kabisa matokeo yaliyotangaza na tume hiyo," alisema Odinga, akieleza kwamba moja ya sababu ni kuwa baadhi ya makamishna wa tume hiyo hawakushirikishwa vilivyo kwenye mchakatio wa uhakiki wa kura.

Odinga alishindwa na Naibu wa Rais William Ruto. kw mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na tume hiyo

Wakenya Jumanne walikuwa wakijiandaa kwa uwezekano wa kipindi cha sintofahamu, baada ya naibu wa rais William Ruto kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais, ambao ulikuwa na ushindani mkali.

Macho yote yalikuwa kwa mpinzani wa karibu wa Ruto, Raila Odinga, ambaye alikuwa anafanya jaribio lake la tano katika kiti cha urais kufuatia uchaguzi wa Agosti 9.

Baada ya siku nyingi kusubiri matokeo kwa wasiwasi, Ruto mwenye umri wa miaka 55 alitangazwa kuwa rais mteule siku ya Jumatatu kwa idadi ndogo ya kura dhidi ya Odinga, kiongozi mkongwe wa upinzani ambaye alikuwa akiungwa mkono na chama tawala kufuatia mabadiliko ya kushangaza ya mirengo ya siasa.

Matokeo ya kura hiyo, yenye amani kwa kiasi kikubwa, yataangaliwa kwa makini kama kipimo cha ukomavu wa kidemokrasia katika taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki ambapo chaguzi zilizopita zilikumbwa na madai ya wizi na umwagaji damu.

Tangazo la matokeo halikusaidia kutuliza jazba katika baadhi ya maeneo, huku tume ya uchaguzi iliyosimamia upigaji kura yenyewe ikigawanyika kuhusu matokeo na waandamanaji katika ngome za Odinga kurusha mawe na kuchoma moto matairi. Kwenye kampeni, Odinga na Ruto walikuwa wameahidi kushughulikia mizozo yoyote mahakamani badala ya mitaani.

XS
SM
MD
LG