Waendesha mashtaka wa serikali kuu nchini Marekani wamemfungulia mashtaka raia wa Kenya kwa kujaribu kutekeleza shambulizi la kigaidi kama lililotokea septemba tarehe 11, 2001 nchini Marekani, kwa niaba ya kundi la kigaidi la Al-shabaab.
Cholo Abdi Abdullah, mwenye umri wa miaka 30, na ambaye alikamatwa nchini Ufilipino mwaka 2019, alisafirishwa hadi Marekani jumanne na kufunguliwa mashtaka ya kupanga kuteka nyara ndege na kuigonga kwa jengo.
Amekanusha mashtaka ya ugaidi wakati wa kikao cha mahakama kilichochukua mda mfupi jumatano na kuzuiliwa gerezani bila kupewa dhamana.
Endapo atapatikana na hatia, huenda akafungwa miaka 20 gerezani.
Wakili wake amekataa kuzungumza na waandishi wa habari.
Waendesha mashtaka wamesema kwamba Abdullah alipata mafunzo ya urubani kati ya mwaka 2017 na 2019 nchini Ufilipino, na kupata leseni ya kuwa rubani wakati akijipanga kutekeleza shambulizi hilo.
Maafisa wamesema kwamba mshukiwa alifanya utafiti namna ya kuteka nyara ndege ya abiria ikiwemo namna ya kupita kwenye mlango wa kuingia sehemu wanapokaa marubani, na habari kuhusu jengo refu zaidi katika mji mkubwa zaidi Marekani.
Waendesha mashtaka wamesema kwamba Abdullah alianza kupanga namna ya kutekeleza shambulizi mwaka 2016 chini ya ualimu wa kamanda wa Al-shabaab ambaye alihusika katika kupanga shambulizi la mwaka 2019 dhidi ya hoteli moja mjini Nairobi, Kenya.