Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 14:58

Raia 2 wa Rwanda wamekamatwa DRC kwa tuhuma za kupanga kuangusha ndege ya rais Tshisekedi


Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) akiwa na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame March 24 2022
Rais wa DRC Felix Tshisekedi (kushoto) akiwa na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame March 24 2022

Uhusiano kati ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Jirani yake Rwanda, umeendelea kuwa mbaya, baada ya serikali ya DRC kutangaza kuwakamata watu wanne kwa madai kwamba walikuwa wanapanga kuangusha ndege ya rais Felix Tshisekedi.

DRC imesema kwamba kati ya waliokamatwa ni raia wa Rwanda, ambao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wanajeshi wa DRC.

Kulingana na serikali ya Jamhuri ya kidemokrais ya Congo, Dr. Juvenal Nshimiyimana na Moses Mushabe, ambao ni raia wa Rwanda, wafanyakazi wa shirika llisilo la kiserikali linalohusika na maendeleo ya afya nchini DRC, walikuwa na ushirikiano na baadhi ya maafisa wa jeshi la Congo, wakipanga njama za kumuua rais wa DRC Felix Tshisekedi kwa kuangusha ndege yake.

Waziri wa mambo ya ndani wa DRC Jean Claude Molipe Mandongo, ameambia waandishi wa habari mjini Kinshasa kwamba raia hao wawili wa Rwanda, pamoja na wengine wawili wa DRC waliokamatwa na kuonyeshwa kwa waandishi wa habari, walikuwa wapelekezi, na wamekuwa wakishirikiana pia na wanasiasa, wafanyabaiashara na baadhi ya mashirika ya kijamii ndani ya DRC.

Msemaji wa jeshi la DRC Sylvian Ekenge, amesema kwamba walipata taarifa muhimu kuhusu usalama kwenye simu ya mmoja wa washukiwa, kwa jina Mushabe, na ushahidi kwamba alikuwa akishirikiana na baadhi ya wanajeshi wa DRC kuangusha ndege ya Tshisekedi.

VOA haijathibitisha madai kwamba Mushabe ni afisa katika jeshi la Rwanda, na kwamba ni mtoto wa kamanda wa jeshi la akiba la Rwanda Generali Eric Murokore.

“Tumewakamata na tumepata ushahidi wa kutosha kwenye simu zao kwamba wamekuwa wakishirikiana na watu kadhaa wakiwemo wanajeshi na wafanyabiashara. Wameunda mikakati yao katika sehemu za Kivu, Kasai, Kivu kaskazini na kivu kusini,” amesema Mandongo.

Majibu ya serikali ya Rwanda

Serikali ya Rwanda imekanusha madai hayo ya DRC.

Rwanda imekuwa ikilalamika kwa muda mrefu kwamba serikali ya DRC imekuwa ikikamata raia wake na kuwazuilia gerezani, ikitaka waliokamatwa kuachiliwa bila masharti yoyote.

Ofisi ya msemaji wa serikali ya Rwanda imesema kwamba Mushabe anaugua na anahitaji matibabu na kwamba kukamatwa kwake ni sehemu ya kile DRC imekuwa ikifanya dhidi ya raia wa Rwanda bila sababu yoyote.

Rwanda imesema kwamba raia wake walioonyeshwa kwa waandishi wa habari walikamatwa mwezi Agosti.

"Dr. Juvenal Nshimiyimana na Moses Mushabe, ambao ni wafanyakazi a shirika la maendeleo ya Afya Afrika wamekuwa wakizuiliwa mjini Kinshasa tangu Agosti 30, 2022 ," imesema taarifa kutoka kwa msemaji wa serikali ya Rwanda, ikiongezea kwamba "viongozi wa DRC wana lengo la kueneza chuki na jumuiya ya kimataifa inastahili kuwaajibisha."

Mgogoro kati ya Rwanda na majirani

Hii sio mara ya kwanza Rwanda inatuhumiwa kwa kupanga njama za ujasusi na kutaka kutataiza usalama katika nchi Jirani.

Imewahi kutuhumiwa na Uganda, Burundi na Tanzania, Japo ilikanusha madai hayo ikisema kwamba waliokuwa wakikamatwa katika nchi hizo walikuwa raia wa Rwanda wasio na hatia yoyote.

Mpaka kati ya Uganda na Rwanda ulifungwa kwa muda mrefu baada ya Uganda kuanzisha msako wa kuwakamata raia wa Rwanda.

Rwanda ilisisitiza kwamba raia wake wengi walikuwa wanazuiliwa katika magereza ya Uganda bila hatia yoyote.

Uganda ilidai kwamba waliokamatwa walikuwa wahalifu, na walikuwa na makosa ya kujibu ikiwemo kuhatarisha usalama wa Uganda.

wafungwa kashaa waliachiliwa na kurudishwa Rwanda.

DRC imekuwa ikishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23, madai ambayo Rwanda imekanusha kila mara.

Ripoti ya umoja wa mataifa ya Mwezi Decemba 2022 imetaja Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23.

Serikali ya Marekani, Ufaransa, Ujerumani, ubelgiji na mashirika maengine yametaka Kigali kukoma kuunga mkono kundi hilo la waasi.

XS
SM
MD
LG