Jimbo la Ituri na jimbo jirani yake la kusini la Kivu Kaskazini zimekumbwa na ongezeko la machafuko kati ya makundi kadhaa ya wanamgambo katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini kwenye mpaka na Uganda.
Kundi moja, CODECO, linasema linalinda jamii ya Walendu dhidi ya kabila lingine la Wahema na vile vile dhidi ya jeshi la Congo.
Wahema hata hivyo, wanalindwa na kundi la wanamgambo liitwalo Zaire, huku jimbo hilo likilengwa pia na waasi wa ADF wenye uhusiano na kundi la kigaidi la Islamic State.
Ofisi ya Umoja wa mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) imeonya kuhusu “mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya raia katika wilaya tatu tofauti, Djugu, Irumu na Mambasa ambayo yameua takriban raia 150 tangu mwanzoni mwa mwezi Aprili.
Matokeo yake ni kwamba, Wilaya ya Irumu “imekuwa kimbilio la maelfu ya watu wanaotoroka ukosefu mkubwa wa usalama”, OCHA imesema.
Mashambulizi pia yameripotiwa kulenga vituo vya afya na huduma nyingine muhimu, Umoja wa mataifa umesema.