"Tuko tayari kushauriana na kila mtu aliyehusika kuhusu suluhu zinazokubalika, lakini ni juu yao. Siyo sisi tunaokataa majadiliano, ni wao,” Putin ameiambia televisheni ya serikali, Rossiya 1, katika mahojiano yaliyopeperushwa Jumapili.
Mshauri wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema Putin anatakiwa kutambua ukweli wa mambo na kukiri kuwa ilikuwa ni Russia ambayo haitaki mazungumzo.
“Russia iliishambulia Ukraine na inaua raia,” mshauri huyo, Mykhailo Podolyal ameandika kwenye Twitter.
Ameongeza kuwa “Russia haitaki mazungumzo, lakini inajaribu kukwepa uwajibikaji wake.”
Uvamizi wa Russia wa Februari 24 ulisababisha mzozo mbaya zaidi barani Ulaya tangu vita vya pili vya dunia na uhasama mkubwa baina ya Moscow na nchi za magharibi tangu mzozo wa makombora wa Cuba mwaka 1962.