Putin amemwambia waziri wake wa ulinzi Sergei Shoigu, katika kikao kilichoonyeshwa kwenye televisheni kwamba wanajeshi wa Russia wanastahili kukizingira kiwanda hicho kiasi kwamba hata nzi asipate nafasi ya kupita, akiongezea kwamba hatua ya kukishambulia kiwanda hicho itawaweka wanajeshi wa Russia katika hatari isiyokuwa na maana yoyote.
Shoigu amemwambia Putin kwamba wanajeshi 2,000 wa Ukraine wamo katika kiwanda cha Azovstal, lakini sehemu nyingine za mji wa Mariupol, ambao ni mji muhimu wenye bandari, umekombolewa na wanajeshi wa Russia.
Zaidi ya watu 100,000 wanaaminika kukwama katika mji wa Mariupol, ambao ulikuwa na wakaazi 400,000 kabla ya wanajeshi wa Russia kuivamia Ukraine Februari 24. Rais wa Marekani Joe Biden anatarajiwa kuzungumzia vita vya Ukraine hii leo Alhamisi, wakati utawala wake unatayarisha msaada mwingine wa kiasi cha dola milioni 800 kwa ajili ya Ukraine.