Kwa mijibu wa shirika la habari la AP, vifaa kama vile kamera pamoja na kofia nyekundu zinazovaliwa na wafuasi wa Wine zilichukuliwa wakati wa msako huo.
David Rubongoya ambaye ni afisa kwenye chama cha Bobi Wine ameiambia AP kwamba kila kitu kilibebwa wakati wa msako huo.
Ripoti zinaongeza kusema kuwa tukio hilo lilifanyika wakati Wine ambaye jina lake kamili ni Kyagulanyi Ssentamu alipokuwa akifanya mkutano na viongozi wengine wa chama chake cha National Unity Platform, ingawa yeye na baadhi ya waliokuwemo hawakukamatwa.
Hata hivyo muda mfupi baadaye, Wine aliandika ujumbe wa Twitter akisema kuwa wafuasi wake wamejeruhiwa kufuatia msako wa polisi kwenye makao makuu ya chama chake.
Hakuna tamko lolote lililotolewa na polisi kufikia sasa. Bobi Wine ananuia kumuondoa madarakani Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 76, na ambaye ametawala Uganda tangu 1986.