Waandamanaji mjini Dakar walichoma matairi na kuchoma moto mabasi na duka kubwa la vyakula ikiwa ni mlipuko wa hivi karibuni wa ghasia ambazo zimeitikisa sifa ya Senegal kama ngome ya demokrasia tulivu kabla ya uchaguzi wa rais mwaka ujao.
Mapambano ya Alhamisi yalianza wakati wafuasi wa mgombea urais Ousmane Sonko walipozuiwa kuandamana na msafara wake hadi mahakamani ambako anakabiliwa na kesi ya kashfa.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 30 baada ya mawakili wa Sonko kusema kwamba alikuwa akitafuta matibabu kutokana kuvuta hewa iliyokuwa na kitu ambacho kilimsababishia kupata shida ya kupumua na kuathiri macho yake.
Sonko, mwenye umri wa miaka 48, ambaye aliibuka wa tatu katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2019, pia anashtakiwa kwa kumbaka mfanyakazi wa saluni mwaka 2021 na kutoa vitisho vya mauaji dhidi yake. Anakanusha makosa yote na anasema shutuma hizo zimechochewa kisiasa ili kumzuia kushiriki katika uchaguzi wa Februari 2024.