Polisi wa Afrika Kusini walisema Ijumaa kuwa wamewaokoa raia 26 wa Ethiopia wasiokuwa na vibali ambao walikuwa wakishikiliwa mateka bila nguo katika nyumba moja mjini Johannesburg na watu wanaoshukiwa kuwa wasafirishaji haramu wa binadamu.
Takriban wanaume wengine 30 pengine tayari wametoroka kupitia dirisha lililovunjwa kabla ya polisi kuivamia nyumba hiyo Alhamisi jioni na huenda wakawa wamejificha katika eneo hilo, kitengo cha uhalifu maalum cha polisi kilisema.
Kulingana na taarifa za awali kutoka kwa watu waliookolewa, kundi hilo lilizuiliwa katika nyumba hiyo katika kitongoji cha Sandringham kaskazini mwa Johannesburg bila nguo wala stakabadhi, Kanali Philani Nkwalase alisema.
Agosti mwaka jana, polisi waliwapata zaidi ya Waethiopia 80 wasio na vibali wakiwa wamefungiwa ndani ya nyumba katika kitongoji hicho hicho katika mazingira ya kinyama na bila chakula cha kutosha wala vifaa vya usafi binafsi.
Forum