Kenneth, mwenye umri wa miaka 52, alishindwa na seneta wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko, kwenye uchaguzi wa mchujo uliofanyika mwishoni mwa mwezi Aprili, kutafuta tikiti ya chama kinachotawala cha Jubilee.
Kenneth alitangaza azma yake alipowahutubia waandishi wa habari mjini Nairobi.
Baada ya uchaguzi huo wa mchujo, Kenneth alilalamikia jinsi ulivyofanyika na kusema kuwa uligubikwa na dosari.
"Sitaki kujihusisha na uchaguzi huo wa Jubilee uliogubikwa na dosari chungu nzima," alisema mwanasiasa huyo mnamo tarehe 27 mwezi Aprili baada ya Sonko kutangazwa mshindi.
Kenneth, ambaye kwa wakati mmoja alikuwa mbunge aliyewakilisha eneo la Gatanga, kaunti ya Murang'a, aliwania urais mwaka wa 2013 lakini akashindwa.
Sasa anatarajiwa kushindana na Mike Sonko, gavana wa sasa wa Nairobi ambaye atawania kiti hicho kwa tikiti ya ODM, Evans Kidero, na mwansiasa mwingine anayesimama kama mgomea huru, Miguna Miguna.