Akizungumza kutokea kwenye roshani ya kanisa kuu la St Peter's Basilica, Papa Francis, mwenye umri wa miaka 86 alianza kwa kuwakumbuka wananchi wa Ukraine akisema "Dada na kaka zetu wanasherehekea Krismasi wakiwa katika giza na baridi,"
"Nina muomba Mwenyezi Mungu atupe imani ya kufanya vitendo thabiti vya kuwasaidia wale wote wanaotaabika, na awapatie busara wale wenye madaraka kunyamazisha dhoruba ya silaha na kukomesha mara moja vita visivyo na maana," alisema Papa Francis.
Mkuu huyo aliyataja mataifa mengi yanayokabiliwa na matatizo wakati huu wa Krismas, ikiwa ni kutokana na vita au mzozo wa kibinadamu, kuanzia Afghanistan hadi Yemen, Syria, Myanmar, ugomvi kati ya Wapalestina na Israel, Lebanon na Haiti.
Kwa mara ya kwanza pia alitoa wito wa upatanishi nchini Iran, nchi inayokumbwa na malalamiko na maandamano yanayoongozwa na wanawake kwa miezi mitatu sasa.
Katika hotuba yake ya Jumapili, Papa Francis aliwahimiza wanaosherekea Krismasi kuwakumbuka wale wanaokabiliwa na njaa, wakati idadi kubwa ya chakula kinatupwa kila siku na rasilimali zinatumiwa kwa ajili ya silaha.
"Vita vya Ukraine vimezidisha hali hii , na kuwaweka watu wengi katika hatari ya njaa, hasa nchini Afghanistan na nchi za Pembe ya Afrika." alisema.
Siku ya Jumamosi usiku Papa Francis aliongoza misa ya Mkesha wa Krismasi kwenye kanisa kuu la St Peter's Basilica akiwa kwenye kiti cha wagonjwa kutokana na maumivu ya magoti.
Maafisa wa Vatican wanasema kuna karibu watu elfu 70 waliohudhuria sherehe za Jumapili na waumini elfu 7 walihudhuria misa ya usiku wa Jumamosi, na mamilioni wakifuatilia kupitia televisheni.