Maelfu ya watu walipunga matawi ya mtende na mzeituni wakati Papa Francis alipokuwa akiingia katika uwanja wa St. Peter akiwa ameketi nyuma ya gari jeupe la wazi kabla ya kuanza kwa Misa iliyochukua saa mbili.
“Ninawashukuru kwa ushiriki wenu na pia kwa sala zenu, ambazo ziliongezeka katika siku zilizopita, ahsanteni,” alisema mwishoni mwa ibada akigusia kuugua kwake hivi karibuni.
Papa huyo mwenye umri wa miaka 86 alipelekwa katika hospitali ya Gemelli mjini Rome siku ya Jumatano baada ya kulalamika kuwa ana matatizo ya kupumua, lakini afya yake ikaimarika baada ya kupata matibabu na akarejea katika makazi yake Vatican siku ya Jumamosi.