Papa Francis amehimiza wale wote wenye mizigo mioyoni mwao kujiweka huru na kujali ubinadamu zaidi kwa kusamehe na kujenga jamii yanye amani.
Katika uwanja wa mashujaa wa Imani mjini Kinshasa, ulifurika raia wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Papa Francis amehimiza vijana, ambao ni kizazi cha Congo ambacho kimekua katika mazingira ya vita, migogoro ya kisiasa na ufisadi, kuwa wenye amani na wakweli kwa kila mmoja.
Hotuba ya papa Francis ilifurahiwa na vijana hao, waliomshangilia kila mara, na kwa wakti mmoja kuwahimiza kushikana mikono kama ishara ya umoja na kuwaambia kwamba kila mmoja anamtegemea mwingine ili kufanikiwa maishani.
Ufisadi na tamaa ya mali
Amewahimiza pia kutojihusisha na madawa ya kulevya, ufisadi au kutafuta mali kwa njia zisizofaa wakitaka kutajirika kwa haraka wala kujiingiza katika vita ambavyo vimekumba mashariki mwa nchi hiyo.
Mapigano yamekuwa yakiendelea mashariki mwa Jmahuri ya kidemokrasia ya Congo kwa muda wa miongo kadhaa. Kuna zaidi ya makundi ya waasi 120 na makundi mengine yanayodai kujilinda kutokana na mashambulizi ya makundi ya waasi.
Karibu watu milioni 6 wamekoseshwa makao. Wakati Papa Francis amekuwa Kinshasasa, mapigano makali yanaendelea kati ya kundi la waasi la M23 l na wanajeshi wa serikali.
Licha ya DRC kuwa na madini yenye thamani kubwa duniani, raia wake wengi ni maskini. Papa Francis amesisitiza kwamba wakati umefika kwa wanaopigana kuweka chini silaha kabisa na kukumbatia huruma, akiongezea kwamba ni kosa kubwa kwa wale wanaojiita wakiristo kuendelea kupigana.
Ujumbe wa msamaha
Kwa walioathirika na vita na migogoro ya DRC, Papa Francis amewataka kusamehe na kuwa wenye matumaini ya kutokea mema, akisisitiza kwamba mwenyezi mungu anajua vidonda vyao, watu wao na nchi yao.
Vatican imesema kupitia ujumbe wa Twiter kwamba zaidi ya watu milioni moja wamehudhuria misa ya papa Francis kwa ajili ya amani na haki mjini Kinshasa.
DRC ni mojawapo ya nchi zenye idadi kubwa ya waumini wa kanisa katoliki duniani.
Kanisa katoliki linajihusisha pakubwa katika maswala ya demokrasia, elimu na afya nchini humo.
Papa Francis anaelekea Sudan kusini, nchi nyingine ya Afrika mashariki ambayo imekumbwa na migogoro na vita tangu ilipopata uhuru.