Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis, amekamilisha ziara rasmi nchini Kenya kwa kuhutubia halaiki kubwa ya vijana katika viunga vya mji mkuu wa Nairobi.
Papa amesema Kenya inakabiliana na tatizo kubwa la rushwa na ukabila ni kama nchi iliyoshikwa na ugonjwa wa kisukari.
Mapema Ijumaa asubuhi, Baba Mtakatifu aliongoza misa takatifu katika mtaa duni wa watu masikini wa Kangemi na baadaye kuhutubia umati mkubwa wa watu katika uwanja wa michezo wa Kasarani.
Katika hotuba yake kwa taifa, Papa Francis aliwalaumu matajiri wanaohusika na rushwa. Amesema tatizo la rushwa linafanana sawa na matumizi makubwa ya sukari ambapo mtu anashindwa kuacha kuitumia kwasababu ni tamu. Hatimaye watu kama hao wanashikwa na ugonjwa wa kisukari, jambo ambalo limeifanya Kenya kuwa mtu au taifa lenye ugonjwa wa kisukari.
Vile vile Baba Mtakatifu ambaye alikuwa akishangiliwa na vijana wakati wote wa hotuba hiyo,amesema Kenya ina tatizo la ukabila ambao lazima kuangamizwa.
Kabla ya kuondoka mjini Nairobi, Papa Francis ameshutumu vikali tabia ya kuwashurutisha vijana kujiingiza katika itikadi kali za kidini kwa manufaa yao wenyewe.
Na tangu Baba Mtakatifu kuwasili nchini Kenya, kumekuwa na mshikamano na maelewano kati ya wanasiasa na wananchi wa tabaka mbali mbali.