Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara anaongoza katika hesabu ya kura katika uchaguzi uliofanyika jumamosi.
Ouattara mwenye umri wa miaka 78, anagombea mhula wa tatu madarakani licha ya maandamano makubwa yaliyotokea kupinga hatua yake ya kugombea mhula mwingine.
Hadi wakati tunaandaa ripoti hii, alikuwa amepata ashindi mkubwa katika wilaya 26 kati ya 108.
Rais Ouattara anatarajiwa kushinda mhula mwingine baada ya wapinzani wake kuambia wafuasi wao kutoshiriki uchaguzi huo wakidai kwamba sio uchaguzi unaokubalika kisheria.
Ouattara amesisitiza kwamba katiba mpya iliyopitishwa mwaka 2016 inamruhusu kugombea mhula mwingine madarakani.
Watu 30 wameuawa katika maandamano ya kupinga Ouattara kugombea mhula mwingine madarakani.
Watu 5 wameripotiwa kuuawa jumamosi wakati uchaguzi ulikuwa unaendelea.
Katika taarifa ya Pamoja, wagombea wa upinzani akiwemo aliyekuwa rais Henri Konan Bedie, na aliyekuwa waziri mkuu Pascal Affi N’Guessan wamesema kwamba watu 30 wameuawa. Hawakutoa taarifa zaidi.
“upinzani unaitisha maandamano kuzuia udikteta huu.” Amesema Affi.
Amesema kwamba asilima 10 ya wapiga kura wameshiriki katika zoezi la upigaji kura, lakini hajatoa Ushahidi wowote.
Hakuna taarifa rasmi kuhusu idadi ya watu ambao wamepiga kura lakini kundi la waangalizi wa ndani limesema kwamba asilimia 23 a vituo vya kupigia kura havikufunguliwa baada ya kuzuiwa na wafuasi wa upinzani waliofunga njia kuelekea kwenye vituo hivyo, na kuwatishia maafisa wa tume ya uchaguzi.
Watu 3,000 waliuawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2010 – 2011 nchini Ivory Coast.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC