Jopo la Umoja wa Mataifa la mabadiliko ya hali ya hewa linasema ongezeko la hali ya joto duniani hivi sasa ni jambo la kudumu katika maisha ya kila siku lakini hatua bado zinaweza kuchukuliwa ili kuzuia athari mbaya.
Jopo la kiserikali juu ya mabadiliko ya tabia nchi lilitoa ripoti Jumatatu iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu likisema mabadiliko ya hali ya hewa yanasababishwa bila shaka na shughuli za kibinadamu ambazo zimepelekea kuongezeka kwa joto duniani kwa zaidi ya nyuzi 1.1 Celsius tangu karne ya 19 kabla ya kuwepo viwanda vingi.
IPCC inaonya kwamba katika muda wa miaka 20 dunia huenda ikafikia na kuvuka kiwango cha joto cha digrii 1.5 za celcius ambacho wanasayansi wametabiri kitasababisha mabadiliko yasiyoweza kurekebishwa kama vile kuyeyuka kwa barafu, kuongezeka kwa viwango vya maji baharini na mafuriko mabaya, pamoja na ukame kote duniani.
Hata hivyo IPCC pia inasema dunia inaweza kupunguza athari za mabadiliko makubwa kupitia kubadili mara moja kwa mafuta, chanzo cha uzalishaji wa hewa ya carbon ambayo inasababisha athari inayoitwa gesi chafu ambapo joto linanaswa katika anga ya dunia, badala ya kutolewa kuingia kwenye nafasi nyingine.