Mwanariadha wa Ethiopia Almaz Ayana ameshinda medali ya dhahabu katika mbio za mita 10000 wanawake kwenye michezo ya Olimpiki Ijumaa huku akiweka rekodi mpya ya dunia ya dakika 29 na sekundu 17.45.
Mkenya Vivian Jepkemoi Cheruiyot alichukua nafasi ya pili na kuipatia Kenya medali ya fedha katika muda wa dakika 29 na sekunde 32.53. Muethiopia mwingine Tirunesh Dibaba alichukua medali ya shaba katika nafasi ya tatu akitumia muda wa dakika 29 na sekunde 42.56.
Ayana wa Ethiopia aliwatoka wenzake kwa mbali ikiwa imebakia mizunguko miwili kumaliza mbio hizo na ilionekana wazi kuwa anaelekea kuvunja rekodi ya dunia.
Cheruiyot ambaye ni mshindani wa siku nyingi wa wanariadha wa Ethiopia alijikuta ametokwa ghafla na Ayana, lakini alijitahidi kushikilia nafasi ya pili na kumwacha Dibaba akishika nafasi ya tatu.
Wakenya wengine wawili walishika nafasi za nne na tano , Alice Aprot Nawowuna akimaliza katika muda wa dakika 29:53.51 akifuatiwa na Betsy Saina aliyemaliza katika muda wa dakika 30:07.78.
Diane Nukuri wa Burundi alimaliza katika nafasi ya 13 katika muda wa dakika 31:28.69, na Salome Nyirarukundo wa Rwanda alimaliza katika nafasi ya 27 katika muda wa dakika 32:07.80.
Cheruiyot amekuwa mwanariadha wa kwanza wa Kenya kuipatia nchi yake medali katika michezo ya Olimpiki ya Rio 2016.