Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 19:01

Odinga awasili mahakamani; uchaguzi urudiwe, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi atimuliwe.


Mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wakati akiasilisha maombi yake kwa mahakama kuu. Anataka mahakama kufutilia mbali ushindi wa Dr. William Ruto kama rais mteule. Aug 22 2022 PICHA: Reuters
Mkuu wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga wakati akiasilisha maombi yake kwa mahakama kuu. Anataka mahakama kufutilia mbali ushindi wa Dr. William Ruto kama rais mteule. Aug 22 2022 PICHA: Reuters

Aliyekuwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu wa Kenya, Agosti 9, Raila Odinga, na muungano wake wa Azimio, wamewasilisha hoja 23 kwenye mahakama ya juu, kutaka ushindi wa Dr. William Ruto ubatilishwe, kwa madai kwamba uchaguzi na hesabu ya kura vilijaa udanganyifu.

Anataka uchaguzi kurudiwa na usisimamiwe na mwenyekiti wa sasa wa Tume ya uchaguzi Wafula Chebukati.

Odinga na mgombea mwenza Martha Karua, pamoja na muungano wa Azimio, wanataka mfumo mzima wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC kufanyiwa ukaguzi wa kina, ikiwemo kuchunguzwa kwa undani zaidi kura ambazo zilikataliwa kujumuishwa kwenye hesabu kamili.

Isitoshe, wanataka ukaguzi huo kufanyiwa fomu zote zilizo na hesabu ya kura.

Raila amedai kwamba tume ya uchaguzi ‘ilimnyima ushindi’

Odinga, na wafuasi wake wanadai kwamba tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, ilihusika katika njama ya kuhakikisha kwamba hashindi uchaguzi huo, kwa kutumia hesabu bandia na kwamba mchakato mzima wa uchaguzi ulijaa dosari.

Mawakili wa Odinga wamewasilisha kile kimetajwa kama ‘ripoti ya uhakiki’ kuhusu wafanyakazi wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, ambao walikuwa na namba au maneno ya siri, na wenye uwezo wa kuingia kwenye mfumo wa digitali wa IEBC, na kuvuruga au kuchakachua daftari la wapiga kura pamoja na kubadilisha majina na vituo vya kupigia kura.

Wiki moja kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, ripoti ya zoezi la uhakiki lililofanywa na kampuni ya KPMG, ambayo ilipewa tume ya uchaguzi IEBC, kabla ya daftari la mwisho la wapiga kura kuchapishwa, ilieleza kuwepo kwa maelfu ya wapiga kura waliokuwa wamesajiliwa zaidi ya mara moja, waliosajiliwa kwa kutumia passpoti ambazo muda wake ulikuwa umemalizika au vitambulisho visivyo rasmi.

Mpango mpana wa Odinga na muungano wa Azimio ni kuieleza mahakama namna ripoti ya ukaguzi wa kampuni ya KPMG ilivyoonyesha kuwepo hali ya kuchakachua daftari la wapiga kura na namna mfumo wa digitali wa kupigia kura ulikuwa mwepesi kudukuliwa na kuvurugwa na mtu yeyote.

Ripoti ya KPMG ilionyesha kwamba kulikuwa na maafisa 14 wa tume ya uchaguzi, wenye jukumu la kujumlisha hesabu ya kura na kutangaza katika vituo vya kupiga kura na maeneo bunge, na ambao hawakuwa wanajulikana, waliokuwa wameingia kwenye mfumo wa digitali wa IEBC, na kwamba walikuwa wanaendelea kuvuruga daftari la wapiga kura kwa hiari.

Ripoti hiyo ilisema kwamba kulikuwepo hatari ya wadukuzi kuingia kwenye daftari la wapiga kura la kidigitali na kwamba kulikuwepo hatari ya kuwanyima wapiga kura haki ya kushiriki zoezi hilo kwa kufuta majina yao kwenye daftari.

Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai awajibike

Maombi ya Raila Odinga kwa mahakama, ni kutaka mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Kenya, George Kinoti awasilishe mahakamani tarakilishi, simu, picha, taarifa za upelekezi, simu na vifaa vingine ambavyo polisi walipata kwa raia wa Venezuela baada ya kuwakamata katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta, siku chache kabla ya uchaguzi mkuu. Raia hao walihusishwa na tume ya uchaguzi IEBC.

IEBC ilisema kwamba raia hao walikuwa wafanyakazi wa kampuni ya kidigitali iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi huo.

Vile vile, Odinga anataka Kinoti kuitwa mahakamani na kutoa taarifa zote kuhusu vifaa walivyopata kwenye ofisi ya wakala wa chama cha United Democratic Alliance UDA, Godfrey Koech Kipngosos, kwenye uvamizi uliofanywa ofisini mwake siku chache kabla ya uchaguzi mkuu.

Sintofahamu kuhusu maafisa wa IEBC waliokamatwa

Mapema mwezi Julai, mwenyekiti wa tume ya IEBC, Wafula Chebukati alitangaza kwamba tume hiyo ilikuwa imewasimamisha kazi wafanyakazi wake watatu, na kuripoti kwa idara ya upelelezi ya makosa ya jinai DCI, ambao walikuwa wanahusika katika kuhamisha wapiga kura kwa njia zisizo halali.

Raila na muungano wake wa Azimio, wanalenga kutumia hii kama shabaha, katika kuieleza mahakama kwamba IEBC haikuchukua hatua za kutosha kuzuia uhamishaji wa wapiga kura kwa njia haramu kuendelea, na kwamba hilo lilichangia pakubwa katika kupunguza kura za Odinga katika maeneo wanayoamini ni ngome zake.

Mawakili wa Odinga vile vile wanahoji kwamba tume ya uchaguzi haikuweka wazi kuhusu maafisa wake wa uchaguzi ambao iliwasimamisha kazi na namna ilizima jaribio kama walilokuwa wanafanya kama lilitokea kwa mara nyingine ili kuzuia udanganyifu katika hesabu ya kura.

Kugawanyika kwa tume ya uchaguzi, makamishna 4 kujitenga na matokeo

Muungano wa Odinga, unalenga kuwasilisha hoja pana zinazogusia sehemu kadhaa za uchaguzi wa Agosti 9, kwa jopo la majaji saba wakiongozwa na jaji mkuu Martha Koome, na kuitaka mahakama hiyo kurudia maamuzi yake, iliyofanya mwaka 2017 ambapo ilifutilia mbali ushindi wa rais Uhuru Kenyatta na kutaka uchaguzi kurudiwa. Odinga hata hivyo alisusia uchaguzi wa marudio mwaka 2017 na kuitisha maandamano.

Odinga atawasilisha kile ambacho mawakili wake wamekitaja kama ushahidi kwamba tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC iligawanyika na hivyo uchaguzi haukuwa huru na haki kulingana na kanuni za IEBC pamoja na katiba ya Kenya.

Wanadai kwamba katika mazingira hayo, isingewezekana matokeo ya uchaguzi kufanyiwa uhakiki wa kutosha, na kwamba kama hilo lingefanyika, Odinga angetangazwa mshindi, na wala sio Ruto.

Mpasuko ulitokea kwenye tume ya uchaguzi saa chache kabla ya mwenyekiti kutangaza mshindi.

Makamu mwenyekiti Juliana Cherera na makamishna wengine watatu, waliitisha kikao na waandishi wa habari katika hoteli ya Serena na kudai kwamba mchakato wa uchaguzi ulikuwa umezingirwa na wingu la giza na kwamba walikuwa wanajitenga na matokeo yaliyokuwa yakitangazwa na mwenyekiti.

Odinga anasema kwamba matokeo yaliyotangazwa na mwenyekiti, aliyekuwa amebaki na makamishna watatu, hayawezi kukubaliwa kisheria kwa sababu tume nzima ya IEBC haikuketi na kuhakiki matokeo hayo kabla ya kutangazwa.

Wakati anatangaza matokeo, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Wafula Chenukati alisema kwamba makamishna wake walikuwa wamepata vitisho vingi na wengine kujeruhiwa, lakini alisimama kidete na kuheshimu katiba kwa kumtangaza mshindi. Afisa mmoja wa tume ya uchaguzi alipatikana ameuawa.

Idadi kubwa ya kura za urais ‘isiyokuwa ya kawaida’

Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, ilimtangaza Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais, akiwa na kura milioni 7.1. Odinga alimaliza katika nafasi ya pili akiwa na kura milioni 6.9. Wagombea wengine wawili Prof George Wajackoya na David Mwaure, hawakufikisha asilimia moja kwa jumla.

Prof George Wajackoya na David Mwaure, walihudhuria hafla ya kutangazwa Ruto kuwa mshindi wa kura za Urais katika ukumbi wa Bomas, Nairobi Kenya. Walikubali kushindwa. Odinga, hakuhudhuria hafla hiyo. Wafuasi wake walijaribu kumzuia mwenyekiti wa IEBC kutangaza matokeo hayo, kabla ya maafisa wa usalama kuingilia kati.

Mawakili wa Odinga wanadai kwamba kulikuwa na idadi kubwa ya wapiga kura isiyo ya kawaida katika sehemu ambazo Ruto alipata kura nyingi kuliko Raila, na kwamba idadi hiyo inatia shaka. Hoja yao ni kwamba magavana, maseneta, wabunge walipata kura chache kuliko mgombea wa rais katika baadhi ya vituo, hivyo wanataka maelezo zaidi wakidai kwamba vifaa vya kidigitali vilitumika kuiba kura.

Odinga anaamini kwamba kuweka fomu za matokeo ya uchaguzi wazi kwa kila mtu lilikuwa kosa

Odinga na mawakili wake vile vile wana msimamo kwamba hatua ya tume ya uchaguzi kuweka wazi fomu zenye matokeo ya uchaguzi kutoka kwenye kila kituo cha kupigia kura, 34A fomu ya kujumulisha katika kila eneo bunge, 34B na fomu yenye kura za jumla za urais 34C, ilikuwa makosa makubwa, na ilitoa fursa kwa wadukuzi kwenye mtandao na wavuti wa IEBC kubadilisha hesabu ya kura. Tume ya uchaguzi ilieleza kwamba iliweka fomu hizo kwenye wavuti wake ili kuhakikisha kwamba shughuli nzima ya uchaguzi inakuwa wazi kwa kila mtu, kulingana na amri ya mahakama ya mwaka 2017.

Odinga, anasema kwamba ujumlishaji wa kura haukukamilika wakati Chebukati alimtangaza Ruto kuwa mshindi wa uchaguzi huo. Mawakili wake wanasema kwamba matokeo ya kura katika maeneo bunge 28 yalikuwa hayajafanyiwa uhakiki.

Maombi ya Odinga vile vile yanataka IEBC kuweka bayana idadi kamili ya wapiga kura waliotumia mfumo wa digitali na namna wapiga kura waliotumia daftari la karatasi walivyotambuliwa. Muungano wa Azimio unadai kwamba mawakala wake walifukuzwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika eneo la mlima Kenya, ambapo Ruto alipata ushindi mkubwa.

Kila upande una mawakili wenye sifa kubwa nchini kenya

Odinga atawakilishwa na mawakili 9, wakiwemo mawakili wenye sifa ya juu na wa muda mrefu nchini kenya Phili Murgor, Prof Tom Ojienda, Pheroze Nowrojee, James Orengo na aliyekuwa mwanasheria mkuu Amos Wako.

Rais mteule Dr. William Ruto naye atawakilishwa na kikosi cha mawakili 7, akiwemo aliyekuwa wakili wa rais Uhuru Kenyatta Fred Ngatia, wakili maarufu Ahmednasir Abdullahi, Adrian Kamotho, Elias Mutuma, Collins Kiprono, Emmanuel Kibet, miongoni mwa wengine.

IEBC ina mawakili sita wakiongozwa na aliyekuwa mwanasheria mkuu Githu Muigai na Eric Gumbo huku muungano wa mawakili Kenya ukiongozwa na wakili Eric Theuri. Kesi itaanza kusikilizwa siku tano baada ya kuwasilishwa mahakamani. Hiyo itakuwa Jumatatu wiki ijayo. Itasikilizwa kwa muda wa siku 3 kabla ya majaji kuandika maamuzi yao. Jopo la majaji 7 lina siku 14 kutoa uamuzi kamili.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG