Rais Barack Obama wa Marekani anasema anaunga mkono kufanyika kwa mageuzi ya Umoja wa Mataifa ambayo yataipa India kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Kauli hiyo ni dalili ya kukubalika kwa India katika jamii ya nchi zenye nguvu duniani. Rais Obama aliliambia bunge la India kuwa Marekani inataka Umoja wa Mataifa unaofanya kazi kwa ufasaha, unaoaminika na wenye uhalali na "hiyo ndio maana" anaunga mkono India kuwa mjumbe wa kudumu katika baraza hilo.
Akizungumza mjini New Delhi Jumatatu Rais Obama pia alisifu India kuwa ni nchi tayari inayoinuka kama taifa lenye nguvu duniani. Alisema uhusiano wa India na Marekani utakuwa muhimu zaidi katika karne hii ya 21.