Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 10:49

Obama aisihi Ethiopia kufanya kazi kwa uwazi zaidi


Rais Barack Obama akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, kwenye mkutano na waandishi wa habari July 27, 2015, Addis Ababa.
Rais Barack Obama akiwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, kwenye mkutano na waandishi wa habari July 27, 2015, Addis Ababa.

Rais Barack Obama alisema Marekani na Ethiopia ni marafiki imara kwenye masuala mengi lakini aliisihi serikali ya nchi hiyo kuwaruhusu waandishi wa habari na vyama vya upinzani kuendesha shughuli zao kwa uhuru.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumatatu akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn, bwana Obama alisifia rekodi ya kiuchumi ya Ethiopia akieleza kwamba nchi hiyo imewaondoa mamilioni ya watu kwenye umaskini na alisema Ethiopia imekuwa na jukumu kubwa katika kupambana na kundi la wanamgambo la Al-Shabaab la nchini Somalia.

Rais Barack Obama
Rais Barack Obama

Rais huyo wa Marekani alisema pia alikuwa na mazungumzo ya wazi na Waziri Mkuu na alisema kufungua njia kwa waandishi wa habari na upinzani kusikika “kutaimarisha badala ya kuzuia” ajenda za chama tawala. Bwana Hailemariam alisema Ethiopia ina nia ya dhati ya kuboresha haki za binadamu na utawala bora. “Nia yetu ya dhati kwa demokrasia ni ya kweli, sio jambo dogo”, alisema Hailemariam.

Makundi ya haki za binadamu yalimuomba bwana Obama kutoa wito wa mageuzi kutoka Ethiopia mahala ambako serikali inadhibiti asilimia 100 ya viti bungeni na kuendelea kudhibiti vyombo vya habari.

Akiwa mjini Addis Ababa, bwana Obama alikutana na viongozi wa Kenya, Uganda, Ethiopia na Umoja wa Afrika kuzungumzia vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini.

Rais Barack Obama
Rais Barack Obama

Kwenye mkutano na waandishi wa habari Rais wa Marekani alisema hali huko Sudan Kusini inazidi kuwa mbaya mno na alisema Marekani na mataifa ya Afrika mashariki watazungumzia nini kinachotakiwa kufanywa ili kupata mkataba wa amani. Alisema Rais wa Sudan Kusini na viongozi wa upinzani wamekuwa wasumbufu na wanaangalia maslahi yao wenyewe badala ya maslahi ya nchi yao.

Bwana Obama ni Rais wa kwanza wa Marekani kutembelea Ethiopia.

XS
SM
MD
LG